News-Details

News >Details

CHUO KIKUU MZUMBE CHAZINDUA KITUO CHA UBORA KWA UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI WA KIBUNIFU

CHUO KIKUU MZUMBE CHAZINDUA KITUO CHA UBORA KWA UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI WA KIBUNIFU

Chuo Kikuu Mzumbe kimezindua rasmi Kituo cha Ubora kwa Ufundishaji na Ujifunzaji wa Kibunifu (Centre of Excellence in Innovative Teaching and Learning - COEITL), katika hafla iliyofanyika Mei 20, 2025, Kampasi Kuu ya Chuo mkoani Morogoro. Uzinduzi huo umeongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William A. Mwegoha, ambapo amepongeza juhudi zilizowezesha kufanikisha kituo hicho kupitia ufadhili wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET). Katika hotuba yake, Prof. Mwegoha alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha Serikali ya Tanzania inashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Mradi wa HEET kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inayoongozwa na Prof. Adolf Mkenda. “Tunatambua pia mchango wa wadau wa maendeleo, washirika wa kitaaluma, wataalamu wa kiufundi, pamoja na timu ya ndani ya Chuo Kikuu Mzumbe waliofanya kazi kwa bidii kuhakikisha ndoto hii inatimia,” alisema Prof. Mwegoha. Akiwahamasisha wanajumuiya wa chuo hicho, Prof. Mwegoha alisema: "Kituo hiki ni kwa ajili yenu. Kifanyeni kuwa sehemu yenu. Fanyeni majaribio na ongezeni wigo wa mipaka ya ufundishaji na ujifunzaji. Kituo kiwe sehemu ya kupanua mwonekano wa Chuo Kikuu Mzumbe, kuongeza ushawishi wake, kuleta hamasa na kugundua mambo mapya.” Alipongeza pia kitengo cha Mawasiliano na Masoko kwa kazi kubwa na nzuri ya kuendelea kutangaza jina la chuo kwa umahiri na ubunifu mkubwa. Kwa upande wake, Dkt. Idda Lyatonga Swai, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe – Taaluma, Utafiti na Ushauri, alisema kuwa kituo hicho kitawezesha utekelezaji wa programu shirikishi za ujifunzaji (blended programmes) kutoka vitivo mbalimbali ili kwenda sambamba na mahitaji ya sasa ya soko la elimu. “Mradi wa HEET umetuwezesha kupata vifaa vya kisasa. Zamani tulitengeneza maudhui huku kelele zikisikika, lakini sasa tuna vifaa vya kisasa na sehemu tulivu ya kufanyia kazi,” alisema Dkt. Swai. Dkt. Perpetua Kalimasi ambaye ni Mkuu wa kituo hicho, alieleza kuwa mwelekeo wa kimkakati wa COEITL ni kuboresha miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji, na kuboresha mchakato mzima wa ujifunzaji. Alisema kituo hicho kina utaalamu katika maeneo kama vile mbinu bunifu za ufundishaji, usanifu wa mitaala, ujifunzaji wa kidijitali, utengenezaji wa maudhui ya vyombo vya habari, na ujifunzaji jumuishi. Alisisitiza kuwa vitengo, skuli na taasisi mbalimbali ndani ya chuo zinaweza kutumia kituo hicho, na kuwataka wanajumuiya wa chuo kukitumia kwa maendeleo ya kitaaluma. Kwa upande wake, Dkt. Proscovia Kamugisha, Kaimu Mtiva wa Kitivo cha Sayansi za Jamii, alisema kuwa kituo hicho ni muhimu sana kwani kinawapa wanafunzi fursa ya kujifunza kwa kutumia mifumo ya kidijitali. “Kituo hiki kimetusaidia sana katika utekelezaji wa mbinu shirikishi za ujifunzaji (blended mode), na tayari tumeshatengeneza programu mbalimbali kupitia kituo hiki,” alisema. Uzinduzi wa kituo hiki unaonesha kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kinapiga hatua ya kasi ya kidijitali katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa kisasa.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None