News-Details

News >Details

ALAT YATOA MHADHARA WA UMMA MZUMBE, YAONESHA NAFASI YAKE KATIKA KUIMARISHA SERIKALI ZA MITAA

ALAT YATOA MHADHARA WA UMMA MZUMBE, YAONESHA NAFASI YAKE KATIKA KUIMARISHA SERIKALI ZA MITAA

Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) imeendesha mhadhara wa umma mnamo tarehe 23 Mei, 2025 katika Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe, ukilenga kuelimisha jamii ya wanachuo kuhusu nafasi ya ALAT katika kuimarisha utawala bora na ufanisi wa serikali za mitaa nchini. Mhadhara huo, ulioratibiwa na Idara ya Menejimenti ya Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Mradi wa HEET, ulifanyika chini ya Mada isemayo “ALAT Mstari wa Mbele katika kupaza sauti ya pamoja kwa ajili ya Jumuiya ya Serikali za Mitaa nchini Tanzania,” ulihudhuriwa na wanafunzi na wanataaluma mbalimbali wa Chuo Kikuu Mzumbe. Mhadhara huo ulifunguliwa rasmi na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Hawa Tundui, ambaye alisisitiza kuwa ALAT ni taasisi muhimu katika kusaidia serikali za mitaa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Alibainisha kuwa historia ya Chuo Kikuu Mzumbe imejikita katika dhana ya kuimarisha serikali za mitaa, kwani chuo kilianza kama Taasisi ya Maendeleo Mzumbe (IDM) na ililenga kuwajengea uwezo watumishi wa umma katika ngazi ya jamii. Awali, Amidi wa Skuli ya Utawala wa Umma na Menejimenti (SoPAM) Dkt. Idda Lyatonga, alieleza kuwa Skuli hiyo imeandaa mhadhara huo kukuza uelewa wa wanafunzi na jamii kuhusu nafasi ya ALAT kwenye kuimarisha ufanisi wa serikali za mitaa. Mhadhara huo uliwasilishwa na Katibu Mkuu wa ALAT Taifa, Bw. Mohamed A. Maje, ambaye alieleza kwa kina majukumu ya ALAT, historia yake, na mikakati ya kuimarisha mahusiano na taasisi za elimu ya juu na taasisi nyingine. Alisisitiza kuwa ALAT ina jukumu la kuwaunganisha viongozi wa serikali za mitaa, kutoa mafunzo, na kuhakikisha kuwa kunakuwepo na jukwaa la pamoja la kujadili changamoto na mafanikio katika ya serikali za mitaa. Baada ya mhadhara huo, kulifanyika mjadala uliohusisha Maswali na Majibu, ukisimamiwa na wataalamu walioambatana na Katibu Mkuu kutoka ALAT. Mjadala huo uliwapa washiriki nafasi ya kujadiliana kwa kina kuhusu masuala ya kiutawala, changamoto katika utekelezaji wa sera, na nafasi ya vijana katika kuchangia mageuzi ya kiutendaji. Mhadhara huu umetajwa kuwa mwanzo wa ushirikiano wa kimkakati kati ya Chuo Kikuu Mzumbe na ALAT, wenye lengo la kuandaa viongozi wa baadae waliobobea katika masuala ya utawala wa umma na maendeleo ya jamii.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None