Chuo Kikuu Mzumbe kimeingia katika ushirikiano rasmi na Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kwa kusaini hati ya makubaliano tarehe 23 Mei 2025, inayolenga kuimarisha maeneo ya tafiti, mafunzo kwa vitendo, na ubadilishanaji wa uzoefu kati ya pande hizo mbili. Makubaliano hayo yalisainiwa rasmi na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha, pamoja na Katibu Mkuu wa ALAT Taifa Bw. Mohamed A. Maje, katika hafla iliyofanyika katika Kampasi Kuu ya Chuo hicho. Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Mwegoha alisema kuwa ushirikiano huo unaonesha dhamira ya Chuo kikuu katika kuchangia maboresho ya utawala bora kupitia elimu na utafiti. “ALAT imebobea katika kujenga uwezo wa watendaji wa serikali za mitaa. Ushirikiano huu utasaidia wanafunzi wetu kupata mafunzo ya vitendo, huku tafiti za Chuo zikichangia maendeleo ya jamii,” alisisitiza Prof. Mwegoha. Kwa upande wake, Bw. Mohamed A. Maje, Katibu Mkuu wa ALAT Taifa, alieleza kuwa makubaliano hayo ni hatua ya kihistoria inayothibitisha dhamira ya ALAT kuimarisha mahusiano na taasisi za elimu ya juu. “Chuo Kikuu Mzumbe kina historia ya kipekee katika kutoa elimu na maarifa kwa watumishi wa serikali za mitaa. Ushirikiano huu utazaa matunda makubwa katika maeneo ya tafiti, mafunzo ya muda mfupi, na ushauri wa kitaalamu kwa mamlaka za serikali za mitaa nchini,” alisema Bw. Maje. Makubaliano haya yanatarajiwa kuleta manufaa kwa pande zote mbili kwa kukuza maarifa, kubadilishana uzoefu, na kujenga msingi imara wa ushirikiano endelevu kati ya taasisi ya elimu ya juu na wadau wa maendeleo ya serikali za mitaa nchini Tanzania.