Mashindano ya Vitivo ya mwaka 2025 Chuo Kikuu Mzumbe yamefunguliwa rasmi Mei 24, 2025 katika viwanja vya michezo vya chuo, yakihusisha michezo mbalimbali kwa lengo la kukuza vipaji, mshikamano na afya miongoni mwa wanafunzi. Mashindano haya yanayojumuisha vitivo na skuli mbalimbali yanachochea ushirikiano, ari ya ushindani na burudani. Katika ufunguzi huo, Mgeni Rasmi alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, ambaye aliwapongeza wanafunzi kwa mwitikio wao, akieleza kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kujenga nidhamu, afya na mshikamano chuoni. “Nawahimiza wanafunzi kuendeleza vipaji vyao kwani michezo ni sehemu ya maendeleo ya kijamii. Uongozi wa chuo utaendelea kuboresha miundombinu ya michezo na viwanja. Naahidi msimu unaofuata kutakuwa na mabadiliko makubwa sana," alisema Prof. Mwegoha. Prof. Mwegoha pia alielezea furaha yake kwa kuwa na timu ya mpira wa miguu ya wanawake chuoni, akiita hilo hatua muhimu ya kuleta usawa katika michezo. “Kuanzishwa kwa timu ya wanawake ni jambo la kihistoria. Tunataka kuona ushiriki wa jinsi zote kwenye michezo. Pia natamani siku moja kuona Chuo chetu kikipeperusha bendera ya Mzumbe ya ushindi kwenye mashindano mbalimbali kitaifa na kimataifa,” alisisitiza. Aidha, alipokea mapendekezo kutoka Wizara ya Michezo ya Serikali ya Wanafunzi,(MUSO) wakipendekeza kuanzishwa kwa kituo maalum cha sanaa na michezo, pamoja na miundombinu rafiki kwa michezo yote. Vilevile, waliomba waongezwe walimu wa michezo mbalimbali ili kusaidia kukuza vipaji na kuimarisha maandalizi ya timu za chuo pia taa kwenye viwanja ili kuwezesha kufanya mazoezi hadi nyakati za jioni. Kwa upande wake, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Fedha, Mipango na Utawala, Dkt. Moses Ndunguru, alieleza kuwa michezo si burudani tu bali ni sehemu ya mafunzo ya maadili na ustawi wa kukuza mshikamano. "nampongeza Makamu Mkuu wa Chuo kwa kuendelea kuwezesha michezo na kuipa kipaumbele kama eneo muhimu kwa maendeleo ya wanafunzi,” alisema Dkt. Ndunguru. Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi, Bw. Alphonce Kauky, alieleza kuwa mashindano hayo ni jukwaa la kukuza vipaji, kuimarisha afya ya akili na kuunganisha wanafunzi wa kada mbalimbali chuoni. “Tunaendelea kushukuru uongozi wa chuo kwa kuwezesha mashindano haya. Tunawatia moyo wanafunzi hasa wanawake kujitokeza kwa wingi,” alisema. Katika siku ya ufunguzi, mechi mbalimbali zilichezwa ikiwa ni pamoja na mpira wa miguu kwa wanawake ambapo timu ya Queens iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ladies, mpira wa miguu kwa wanaume kati ya Staff na Kitivo cha Sheria (Law) ambao ulimalizika kwa sare ya bila kufungana, pamoja na mpira wa kikapu kati ya Staff na Skuli ya Biashara (SoB) ambapo SoB waliibuka washindi. Mashindano haya yalianza Mei 17 na yanatarajiwa kufikia tamati Juni 1, 2025, yakihusisha michezo ya aina mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, riadha na kadhalika. Ushiriki mkubwa wa wanafunzi unaonyesha dhamira ya kweli ya Chuo Kikuu Mzumbe katika kukuza vipaji na kuendeleza michezo kama sehemu ya maendeleo jumuishi ya kitaaluma na kijamii.