Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Mradi wa Elimu ya Juu na Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kimeendesha Warsha ya kuwasilisha matokeo ya utafiti kwa wadau mbalimbali ambao wana mnasaba na tafiti zilizofanywa. Warsha hiyo inalenga kuwasilisha na kujadili matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanywa na watafiti kutoka Chuo hicho, pamoja na kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ili kutatua changamoto za kitaaluma, kijamii ma kiuchumi. Washiriki wa Warsha hiyo ni wadau kutoka sekata mbalimbali kama vile elimu, afya, sheria, uchumi, nk. Warsha hiyo iliyofanyika tarehe 26 Mei 2025, ilifunguliwa rasmi na Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri Dkt. Joseph Sungau, ambaye alisisitiza umuhimu wa tafiti zenye tija na zenye kuleta mchango halisi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Aidha, alitoa wito kwa watafiti kuzingatia changamoto za wakati huu na kuhakikisha kuwa tafiti zao zinaakisi mahitaji halisi ya jamii. “Ninapenda kuwapongeza wanataaluma wetu kwa juhudi zenu na mchango mkubwa katika kuinua sifa ya utafiti wa Chuo Kikuu Mzumbe. Kazi yenu ni kiungo muhimu katika kuhakikisha kwamba elimu tunayotoa haibaki katika maktaba pekee, bali ina mchango halisi katika kutatua matatizo ya jamii na kuleta mabadiliko chanya. Hivyo, suala la uwasilishaji wa matokeo ya utafiti wenu yanastahilli kuwasilisha kwa wadau Alisisitiza Dkt. Sungau Awali, Kaimu Mratibu wa HEET upande wa Kukuza Uwezo wa Utafiti na Ubunifu Tumishi Prof. Mackfallen Anasel, aliwakaribisha wajumbe kwenye Warsha ya kuwasilisha matokeo ya tafiti zilizofanywa na wanataaluma kutoka Chuo Kikuu Mzumbe. Prof. Mackfallen alibainisha kwamba tafiti hizi zimefadhiliwa na Chuo Kikuu Mzumbe kupitia fedha zake za ndani ikiwa ni juhudi za Chuo Kikuu Mzumbe kuongeza jitihada katika tafiti na machapisho. Pia, alitoa shukrani kwa Mradi wa HEET kwa kufadhili gharama za Warsha hiyo. ”Juhudi zetu za leo hazina thamani kama zitaishia hapa. Ni mwanzo wa safari ndefu ya kuhakikisha kwamba utafiti wetu unakuja na suluhu za changamoto mbalimbali katika Taifa letu,” alisisitiza Prof. Mackfallen. Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utafiti, Machapisho na Masomo ya Shahada za Uzamili, Dkt. Nsubila Isaga alieleza kuwa warsha hiyo ni jukwaa mahususi kwa ajili ya kuwasilisha matokeo ya tafiti zinazolenga kuchangia maendeleo ya Chuo Kikuu Mzumbe na Taifa kwa ujumla. Dkt. Isaga alisisitiza kuwa, ushirikiano baina ya Chuo na Wadau ni nguzo muhimu katika kuhakikisha kuwa tafiti zina tija na zinagusa mahitaji halisi ya jamii. Aidha, Dkt. Isaga alibainisha kwamba warsha hiyo ina jumla ya tafiti kumi na sita (16) na washiriki takribani 133. Dkt Isaga alitoa shukrani kwa wadau wote walioitikia mwaliko na kuonesha utayari wao wa kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya kitaaluma na utoaji wa maoni ya kitaalamu yatakayosaidia kuboresha mwelekeo wa tafiti zijazo. Baada ya ufunguzi wa warsha hiyo, washiriki walijigawa katika makundi mbalimbali kulingana na nyuga ambazo tafiti hizo zimaemakikinia, kama vile kundi la wadau wa Elimu, Mazingira, Afya, Sheria n.k. ili kuwasilisha tafiti hizo na kuzijadili. Baada ya uwasilishaji na majadiliano, wadau walioshiriki kutoka sekta mbalimbali walikipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuwashirikisha katika suala hili. Walisema kwamba suala la kufanya tafiti na kuwashirikisha wadau matokeo yake ni jambo la msingi sana ambalo lingetakiwa kufanywa na taasisi zote za elimu ya juu.