Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha amekutana na kufanya mazungumzo na watumishi wa Chuo hicho Ndaki ya Mbeya ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kutembea ndaki za Chuo kujadili mambo ya kimkakati na maendeleo ya chuo. Prof. Mwegoha akiambatana na sehemu ya Menejimenti ya Chuo hicho kutoka Kampasi Kuu amefanya ziara hiyo tarehe 26 Mei 2025 ambapo amepata fursa kusikiliza changamoto zinazoikabili watumishi wa Ndaki ya Mbeya na kuzitatua. Katika kikao hicho, Prof. Mwegoha amepongeza uongozi wa Ndaki ya Mbeya kwa kuandika miradi mbalimbali, kushiriki katika tafiti na kuwataka kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya Mpango Mkakati wa Chuo sita ambao umeanza kuhuishwa. “Nawapongeza kwa kuandaa utaratibu wa kuwa na mawasilisho ya kila mwezi ikiwa ni hatua ya kujengeana uwezo katika nyanja za taaluma. Natambua hii imewawezesha kushinda maandiko sita kati ya 17 ya Miradi midogo ya Utafiti "small grants" kwa lengo la kuongeza machapisho” Amesisitiza Prof. Mwegoha. Vilevile, amesisitiza kuhusu kufungua chuo kimataifa kwa kuongeza ushirikiano na vyuo mbalimbali nje ya nchi kwa lengo la kubadilishana uwezo Katika kikao hicho, Makamu Mkuu wa chuo alifafanua utekelezaji wa mpango mkakati wa Chuo hususani kipengele cha uendelezaji wa miundombinu na uboreshaji wa mazingira ya kujifunza na kufundishia pamoja na kutoa rai kwa watumishi hao kuhakikisha wanajiendeleza zaidi kimasomo kwa kutumia fursa zilizopo. Aidha, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Hawa Tundui Petro amewataka watumishi kufanya kazi kwa weledi na uzalendo wa hali ya juu ili kuleta tija kwa jamii. Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Prof. Allen Mushi amesema Chuo kinaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika ndaki zote kwa lengo la kuimarisha mazingira ya kujifunza na kujifunzia. Ndaki ya Mbeya ina jumla ya wafanyakazi Mia Moja Thelathini na Nane (138). Wafanyakazi wanataaluma sabini na nane (78) wanaume ni arobaini na tisa (49) na wanawake ishirini na tisa (29). Aidha idadi ya wafanyakazi waendeshiji ni sitini (60) ambapo wanaume ni ishirini na tisa (29) na wanawake ni thelathini na moja (31).