Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha amefanya ziara ya kikazi Ndaki ya Mbeya na kuzungumza na wanafunzi tarehe 26 Mei 2025. Lengo likiwa ni kukagua maendeleo ya wanafunzi, kusikiliza maoni na changamoto kutoka kwa wanafunzi pamoja na kutoa dira na mwelekeo wa Chuo kuhusu masuala muhimu yanayohusu elimu, mazingira na miundombinu bora ili kuhakikisha kuwa Ndaki ipo salama. Akizungumza katika kikao hicho, Prof. Mwegoha alisisitiza wanafunzi kuwa na uzalendo na Chuo kwa kukilinda na kuwajibika kuishi tunu za Chuo Kikuu Mzumbe. “Uzalendo ni jambo muhimu, ukiharibu jina la Chuo hata na wewe binafsi utakuwa umeharibu taswira yako kwa namna moja au nyingine. Linda jina na Chapa ya Chuo ambayo ni kubwa na inayoheshimika ndani na nje ya nchi yetu”, alisema Prof. Mwegoha. Aidha, Prof. Mwegoha alitumia kikao hicho kumtambulisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo -Taaluma, Tafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui kwa wanafunzi wa Ndaki ya Mbeya ambaye ni ziara yake ya kwanza kwa Ndaki tangu apate nafasi hiyo. Prof. Hawa alisisitiza kuhusu umuhimu wa kufuata miongozo ya Chuo Kikuu Mzumbe ili waweze kuhitimu masomo yao vizuri, matumizi sahihi ya Akili Unde (AI), kuwa na nidhamu na uwajibikaji. Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe - Mipango, Fedha na Utawala Prof. Allen Mushi alieleza kuhusu miradi iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa na Chuo kwa Ndaki ya Mbeya ikiwemo Mradi wa Zahanati, Barabara za Ndani na Ukarabati wa Mabweni, Viwanja vya Michezo na Visima vya maji. Aliongeza kuwa wanafunzi wawe walinzi wa miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu. Katika kikao hicho, wanafunzi walipongeza jitihada za uongozi wa chuo katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kisha kutoa maoni na mapendekezo; ikiwa ni pamoja na kuendelea kuboresha miundombinu ya TEHAMA na Maktaba kwa ajili ya ustawi kitaaluma. Akito neno la shukrani kwa niaba ya wanafunzi wote, Rais wa Serikali ya Wanafunzi Ndaki ya Mbeya anayemaliza muda wake Bw. Julius Nyassa alitumia nafasi hiyo kumtambulisha Rais Mteule wa serikali hiyo Bw. Mifolino Maiko kwa Menejimenti, watumishi na wanafunzi, kisha kuomba wampe ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.