Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Mradi wa Elimu ya Juu na Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), kimeendesha warsha maalum ya siku mbili kuanzia tarehe 27 hadi 28 Mei 2025, Hoteli ya Morena yenye lengo la kuwawezesha watafiti na wahadhiri wake kuandika mapendekezo ya miradi ya utafiti yenye uwezo wa kupata ufadhili mkubwa kutoka kwa taasisi za kitaifa na kimataifa. Warsha hiyo imewaleta pamoja watafiti kutoka vitivo mbalimbali vya chuo hicho ili kuwajengea uwezo wa kitaalamu katika uandishi wa maombi ya ruzuku, mbinu za kutambua fursa za ufadhili, na jinsi ya kuandaa bajeti za utafiti zinazokidhi matarajio ya wafadhili. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt.Lihoya Chamwali alisema kuwa warsha hii ni sehemu ya juhudi za chuo kuhakikisha kuwa tafiti zinazofanywa na watafiti wa Mzumbe zina mchango chanya katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia matumizi ya ushahidi wa kisayansi. “Kupitia mradi wa HEET, tunalenga si tu kuimarisha miundombinu na mitaala ya elimu ya juu, bali pia kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwa watafiti ili waweze kufikia viwango vya kimataifa katika ushindani wa ufadhili wa tafiti kubwa,” alisema Dkt. Chamwali. Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utafiti, Machapisho na Masomo ya Uzamili Dkt. Nsubila Isaga, alisisitiza umuhimu wa uvumilivu na ustahimilivu katika mchakato wa kutafuta ufadhili wa tafiti. “Ni muhimu kuelewa kuwa si kila pendekezo la utafiti litapata ufadhili kwa mara moja. Lakini hilo halipaswi kuwakatisha tamaa watafiti. Endeleeni kujaribu, msichoke siku moja utafanikiwa. Wekeza muda wako katika kutafuta na kuboresha mapendekezo yako kila wakati,” alisema Dkt. Isaga. Kwa upande wake, Kaimu Mratibu wa Mradi wa HEET upande wa Kukuza Uwezo wa Utafiti na Ubunifu Tumishi, Prof. Mackfallen Anasel aliwashukuru waandaaji wa warsha hiyo kutoka Kurugenzi ya Utafiti, Machapisho na Masomo ya Uzamili (DRPS) pamoja na Mradi wa HEET kwa kufanikisha kwa ufanisi utekelezaji wa mpango mkakati wa Chuo Kikuu Mzumbe wa kuimarisha shughuli za utafiti. “Nawapongeza DRPS kwa kushirikiana na mradi wa HEET kwa kuandaa warsha hii muhimu inayotekeleza dhamira ya chuo ya kuhakikisha tafiti zinafanyika na kuleta matokeo chanya. Tafiti ni kichocheo kikubwa cha maendeleo, na zina faida kubwa siyo tu kwa chuo, bali pia kwa jamii na taifa kwa ujumla,” alisema Prof. Anasel. Mwezeshaji katika warsha hiyo, Prof. Frank Theobald aliwafundisha watafiti mbinu mbalimbali za kubuni na kuendesha tafiti zenye tija, zinazoweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii. “Ni muhimu kwa watafiti kuelewa muktadha wa changamoto za kijamii na kiuchumi, na kutumia mbinu za kisayansi katika kutafuta majibu. Tafiti zenye tija huanzia kwenye wazo sahihi, muundo thabiti wa utafiti, na utekelezaji makini,” alisisitiza Prof. Theobald. Kwa kushirikiana na Mradi wa HEET, Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kuwekeza katika maendeleo ya kitaaluma na kitaalamu ya watafiti wake ili kuhakikisha tafiti zinazofanyika siyo tu zenye ubora wa kimataifa, bali pia zinaakisi mahitaji ya maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.