News-Details

News >Details

WANAFUNZI WA CHUO KIKUU MZUMBE WAJENGEWA UWEZO KATIKA UBUNIFU

WANAFUNZI WA CHUO KIKUU MZUMBE WAJENGEWA UWEZO KATIKA UBUNIFU

Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), chini ya Kitengo cha Ubunifu, Ujasiriamali na Mahusiano ya Kitasnia, kimeandaa warsha ya siku tano kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa ubunifu kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe – Kampasi Kuu. Warsha hiyo ilianza rasmi tarehe 19 Mei 2025 na inatarajiwa kukamilika tarehe 23 Mei 2025. Akifungua warsha hiyo, Mratibu wa Mradi wa HEET katika Chuo Kikuu Mzumbe kwa upande wa Kujenga Uhusiano kati ya Sekta ya Elimu na Sekta Binafsi/Viwanda, Dkt. Albogast Musabila alisema kuwa lengo la warsha hiyo ni kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuwa na bunifu zitazoleta suluhisho kwenye uhitaji wa jamii, kutengeneza bidhaa au huduma zinazoweza kuleta mageuzi ya kiuchumi, na kuwaandaa kuingia kwenye soko la ajira kwa ushindani mkubwa. “Tunataka kuandaa kizazi cha wahitimu wenye ubunifu wa hali ya juu, walio tayari kutumia ujuzi na maarifa yao kubadilisha jamii na kuchangia katika maendeleo ya taifa. Warsha hii ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wanafunzi wanakuwa si tu wataalamu, bali pia wabunifu na wajasiriamali mahiri,” alieleza Dkt. Musabila. Akizungumza na washiriki wa warsha hiyo, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Bw. Lwako Lubida, aliwasilisha mada kuhusu Misingi ya Ubunifu, akisisitiza umuhimu wa kuwa na fikra pana, ujasiri wa kuchukua hatua, pamoja na uwezo wa kutambua fursa katika changamoto mbalimbali zinazowazunguka. Naye Mhadhiri wa Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Lukiko Lukiko, aliwasilisha mada kuhusu Hati Miliki, akieleza kwa kina maana yake, aina zake na umuhimu wake katika biashara na ujasiriamali. “Yeyote anayetaka kumiliki biashara au bunifu ni lazima ajifunze kwa bidii na kuwa na uelewa mpana kuhusu sheria za mali miliki ili kuweza kulinda ubunifu na bidhaa anazomiliki. Hii ni pamoja na kupitia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), ambao wanahusika na usajili wa makampuni, majina ya biashara, alama za biashara na huduma, pamoja na utoaji wa leseni za viwanda. Ni muhimu kwa wanafunzi kuelewa namna ya kulinda bunifu zao, biashara, na bidhaa walizonazo au zitakazokuja,” alisisitiza Dkt. Lukiko. Warsha hiyo ilihitimishwa na Mratibu wa Ubunifu kutoka Kitengo cha Ujasiriamali na Mahusiano ya Kitasnia, Dkt. Irene Isibika, ambaye aliwapongeza washiriki kwa ushiriki wao mzuri na kuwahimiza kuendelea kutumia fursa kama hizo kujiendeleza kielimu, kiujuzi na kibiashara. Chuo Kikuu Mzumbe, Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu.

None
None
None
None
None
None
None
None
None