Chuo Kikuu Mzumbe kimeandaa mafunzo ya uthibiti ubora kwa wakuu wa idara za taaluma, waratibu wa uthibiti ubora na waratibu wa programu za kitaaluma, yaliyofanyika Kampasi Kuu, mkoani Morogoro na kujumuisha wawakilishi kutoka Kampasi za Mbeya na Dar es Salaam. Mafunzo hayo yaliyofunguliwa rasmi tarehe 26 Mei 2025 na Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Dkt. Joseph Sungau, yamelenga kuwajengea na kuukuza uwezo wa washiriki ili waendane na mabadiliko ya Sera mpya ya Elimu, miongozo ya Kimataifa ya Uthibiti Ubora na mabadiliko ya Kiteknolojia katika uandaaji na uboreshaji wa mitaala. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Dkt. Sungau alisema kuwa katika mazingira ya sasa yenye mabadiliko ya haraka ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira, ni muhimu kwa taasisi za elimu ya juu kuhakikisha kuwa mitaala inayotolewa ni shirikishi, bunifu na yenye kujibu changamoto halisi za jamii. Aliongeza kuwa kupitia mafunzo haya, washiriki wataweza kuimarisha mbinu bora za kuandaa na kuboresha mitaala inayokidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa kitaifa na kimataifa. Naye Mkuu wa Kitengo cha Uthibiti Ubora wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Lawrencia Mushi, alieleza kuwa mafunzo haya ni endelevu na ni sehemu ya maandalizi ya chuo hicho katika kuhakikisha kuwa watendaji wake wanafikia viwango stahiki vya ubora vya kitaaluma wakati wa kuandaa na kupitia mitaala. Alisema hatua hii inalenga kuwawezesha washiriki kuelewa kwa kina mabadiliko ya miongozo barani Afrika ili kuweza kuhuisha mitaala ya Chuo Kikuu Mzumbe kwa kiwango cha juu kitakachowezesha Chuo kupata wanafunzi na walimu wa Kikanda na Kimataifa. Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Prof. Jennifer Sesabo kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, aliwasilisha mada kuhusu Uthibiti Ubora katika Elimu ya Juu, ambapo alieleza kuwa suala la ubora katika taasisi za elimu ya juu linapaswa kupewa kipaumbele ili kuzalisha wahitimu bora na wenye ushindani wa kimataifa. “Taasisi ya elimu ya juu inapotanguliza ubora, huandaa wahitimu wenye uwezo wa kushindana katika soko la dunia. Ubora si tukio moja, bali ni mchakato endelevu unaohitaji dhamira, uwajibikaji na maboresho ya mara kwa mara,” alisisitiza Prof. Sesabo. Mafunzo hayo yanatolewa kwa muda wa siku mbili na yamehusisha washiriki kutoka ndaki zote tatu za Chuo Kikuu Mzumbe, yakiwa ni sehemu ya jitihada za chuo hicho kuhakikisha kuwa mitaala yake inaendelea kuakisi mahitaji ya soko la kitaifa na kimataifa.