Tarehe 28 Mei, 2025, Rasi wa Ndaki ya Mbeya, Prof. Henry Mollel alizindua Mfululizo wa Semina za Uwasilishaji wa tafiti. Tukio hili kubwa linalenga kujenga jukwaa muhimu la kuwasilisha mapendekezo ya tafiti, kukuza utamaduni wa kutoa tafiti na machapisho bora miongoni mwa wanafunzi wa Ndaki ya Mbeya na Chuo Kikuu Mzumbe kwa ujumla. Prof. Henry Mollel, Rasi wa Ndaki ya Mbeya amesema kuwa Mfululizo wa Semina hizi utaweza kuboresha uandishi wa tafiti kwakuwa ni jukwaa litakalotoa mbinu bora za uandishi wa tafiti na uchapishaji wa machapisho katika majarida ya kitaifa na kimataifa. Naye, Prof. Charles Tundui, Naibu Rasi wa Ndaki ya Mbeya amesisitiza wanazuoni na wanafunzi kuhudhuria semina hizi ili kuweza kujifunza na kuwasilisha madoroso, mapendekezo ya tafiti kwa wataalamu wengine. Kupitia semina hizi washiriki wataweza kukuza ubunifu kupitia kubadilishana mawazo kuhusu changamoto na fursa katika maeneo muhimu ya tafiti. Katika uzinduzi huo, mapendekezo ya tafiti mbili yaliwasilishwa kutoka kwa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili Chuo Kikuu Mzumbe pamoja pendekezo la tafiti moja kutoka kwa Mhadhiri Msaidizi ambapo mawasilisho hayo yalifuatia na majadiliano kwa kina na washiriki wa semina hiyo. Ndaki ya Mbeya inapenda kuwaalika wote kuhudhuria semina hizi kwa ajili ya kujifunza kwa maendeleo ya watu.