News-Details

News >Details

CHUO KIKUU MZUMBE KIMEENDESHA MHADHARA WA UMMA KUHUSU UENDESHAJI WA MFUMO WA UNUNUZI WA KIELEKTRONIKI SERIKALINI

CHUO KIKUU MZUMBE KIMEENDESHA MHADHARA WA UMMA KUHUSU UENDESHAJI WA MFUMO WA UNUNUZI WA KIELEKTRONIKI SERIKALINI

Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Skuli ya Biashara (SoB), chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), kimeendesha Mhadhara wa Umma tarehe 30 Mei, 2025 Kampasi Kuu Morogoro. Mhadhara huo uliwalenga wafanyakazi na wanafunzi, hususan wa fani ya Ununuzi na Ugavi, kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu namna serikali inavyotekeleza ununuzi wa umma kwa njia ya kidijitali kupitia mfumo wa kielektroniki wa NeST (National e-Procurement System of Tanzania). Akifungua rasmi Mhadhara huo, Amidi wa Skuli ya Biashara, Dkt. Gabriel Komba, alisema kuwa teknolojia ya kidijitali imeleta mageuzi makubwa katika mnyororo wa ununuzi wa umma, hivyo ni muhimu kwa wanafunzi kujifunza kwa undani kuhusu mifumo hiyo mapema wakiwa vyuoni. “Tunapenda wanafunzi wetu wajifunze kwa vitendo namna teknolojia inavyotumika katika manunuzi ya umma, ili wanapohitimu wawe na uelewa wa kutosha wa mifumo ya kisasa,” alisema Dkt. Komba. Mwezeshaji wa Mhadhara huo Bw. Gilbert Kamnde, Meneja wa Kujenga Uwezo na Huduma za Ushauri kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), alieleza kuwa mfumo wa NeST umebuniwa na wataalamu wazawa na umeiwezesha serikali kutangaza tenda, kupokea zabuni, na kufanya uchambuzi kwa njia ya uwazi na ufanisi. “Faida kubwa ya mfumo huu ni uwazi na uwezo wa kuchuja wazabuni wasio na sifa. Taasisi zote za serikali zimesajiliwa katika mfumo huu ambao unadhibiti mianya ya upendeleo na kuongeza thamani ya fedha za umma,” alisema Bw. Kamnde. Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Ununuzi na Usimamizi wa Usafirishaji Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Paul Nsimbila Kabelele, ambaye alifunga rasmi mhadhara huo, alisisitiza umuhimu wa kuandaa mijadala ya aina hiyo mara kwa mara ili kuimarisha uelewa wa wanafunzi. “Tunathamini mchango wa wadau kama PPRA katika kujenga uwezo wa wanafunzi wetu. Tunatarajia wanafunzi watachukua maarifa haya kwa uzito na kuyaweka katika vitendo,” alisema Dkt. Kabelele. Mhadhara huu ni sehemu ya mikakati ya Chuo Kikuu Mzumbe ya kuwajengea wanafunzi maarifa ya kisasa yanayohitajika sokoni, hasa katika sekta ya ununuzi na usimamizi wa ugavi, ili kuhakikisha wanapohitimu wanakuwa na ujuzi unaochochea maendeleo ya taifa.

None
None
None
None
None
None
None
None
None