News-Details

News >Details

MAKAMU MKUU WA CHUO KIKUU MZUMBE AZUNGUMZA NA WAFANYAKAZI KUHUSU MAFANIKIO NA MIPANGO YA MAENDELEO YA CHUO

MAKAMU MKUU WA CHUO KIKUU MZUMBE AZUNGUMZA NA WAFANYAKAZI KUHUSU MAFANIKIO NA MIPANGO YA MAENDELEO YA CHUO

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Profesa William Mwegoha amekutana na kuzungumza na wafanyakazi wote wa Kampasi Kuu Morogoro ambapo alielezea mafanikio mbalimbali yaliyopatikana chuoni hapo ikiwemo ongezeko la wafanyakazi, marekebisho ya miundombinu mbalimbali ya Chuo ikiwemo uboreshaji nyumba za wafanyakazi, barabara za ndani na uwekaji wa taa za barabarani. Akifungua kikao hicho tarehe 2 Juni 2025, Makamu Mkuu wa Chuo Profesa William Mwegoha amezungumzia kuhusu maendeleo makubwa yaliyopatikana kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET). Ameeleza kuwa mradi huo ni wa kwanza kwa ukubwa tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho kwani una thamani ya takribani shilingi bilioni 49 za Kitanzania na unatekeleza ujenzi wa jengo jipya la kisasa la taaluma na jengo la TEHAMA. Prof. Mwegoha amebainisha kwamba mafanikio mengine yaliyotokana na Mradi huo ni kuboresha na kuhuhisha mitaala,pamoja na ujenzi wa Kampasi mpya ya Tanga katika wilaya ya Mkinga. Vilevile, Prof. Mwegoha amegusia juu ya mpango wa uwekezaji ili kuongeza uwezo wa chuo kujitegemea ambao tayari umeshapitishwa na Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe; hivyo, amewapongeza wafanyakazi kwa ushirikiano wanaompatia. “Utulivu tulionao na kuweza kufanya kazi zetu kwa ubora, inaonesha kuwa tuna umoja thabiti; hivyo, ninapenda kuwapongeza sana wafanyakazi wenzangu,” alisema Prof. Mwegoha. Vilevile, Makamu Mkuu wa Chuo alipata fursa ya kumtambulisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma, Utafiti na Ushauri Profesa Hawa Tundui Petro ambaye baada ya utambilisho aliwashukuru wafanyakazi wote kwani alisema wamehusika kwa namna moja au nyingine katika uteuzi wake. "Tufanya kazi kwa ushirikiano na upendo baina ya wanataaluma na wafanyakazi waendeshaji kwani wote tunategemeana; pia, tuwe wazalendo kwa Chuo chetu na kufanya kazi kwa bidii na uadilifu kwani uadilifu ni mtaji," alisisitiza Prof. Tundui. Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi alisisitiza kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha malengo katika Mpango Mkakati wa Chuo (CSP) ili kuleta maendeleo kwa Chuo. Aliongeza kuwa ni mpango wa Chuo kuwekeza kwenye miradi mbalimbali kuongeza kipato na kuweza kujitegemea. Sambamba na hilo, amewaasa wafanyakazi kuchukua tahadhari na kujilinda dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO-19 na Mpox. Naye Mkurugenzi wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu Chuo Kikuu Mzumbe, Bi. Sophia Mchomvu alielezea kuwepo kwa kibali cha kuajiri wafanyakazi 78. Pia, alitoa msisitizo katika kuzingatia masuala ya kiutawala na maadili ikiwa ni pamoja na ujazaji wa taarifa za kazi katika Mfumo wa Upimaji Utendaji Kazi wa Watumishi 'PEPMIS'. Kikao hicho cha Makamu Mkuu wa Chuo na wafanyakazi kiliwapa nafasi wafanyakazi kuzungumza changamoto mbalimbali, kutoa maoni na ushauri kwa Makamu Mkuu wa Chuo, ambapo aliyepokea maoni hayo na kuahidi kushirikiana na viongozi wenzake kuyafanyia kazi vema. Aidha, katika mkutano huo, Makamu Mkuu wa Chuo alitoa nafasi kwa Kiongozi wa Mfuko wa Faraja kuuelezea mfuko huo kwa wafanyakazi wapya na kuwashawishi kujiunga na katika mfuko huo kutokana na umuhimu wake hususan katika kufarijiana pale mfanyakazi anapofiwa na ndugu wa karibu au anapofariki mfanyakazi mwenyewe. Vivile, nafasi ilitolewa kwa Mkurugenzi wa Huduma za Afya kwa ajili ya kueleza masuala ya msingi ikiwa ni pamoja na kujikinga na Ugonjwa ya kuambukizwa kama vile UKIMWI, kupata kinga ya ugonjwa wa ini, na kujikinga na UVIKO -19. Pia, Prof. Mwegoha alipata nafasi ya kutoa vyeti kwa wafanyakazi bora na hodari wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa upande wa Waendeshaji na Wanataaluma. Vilevile, na yeye (Prof. Mwegoha) alipokea Tuzo ya usimamizi bora wa rasilimali kwa niaba ya wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe kutoka kwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Mipango, Fedha na Utawala Prof. Allen Mushi. Tuzo hiyo ni ya kitaifa, Mzumbe kiliibuka kinara miongoni mwa vyuo vikuu vikuu na vyuo vya kati vyote nchini Tanzania katika weledi wa usimamizi bora wa rasilmali watu.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None