Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa William Mwegoha, amekutana na wanafunzi wa Kampasi Kuu ya Morogoro tarehe 2 Mei 2025 kwa lengo la kuwasikiliza, kupokea maoni na kuwapa mrejesho kuhusu masuala ya kitaaluma, kijamii na kiutawala. Mkutano huu ni sehemu ya juhudi za uongozi wa Chuo kuimarisha mawasiliano na ushirikiano na wanafunzi. Prof. Mwegoha amesema kuwa Chuo kinaendelea kuimarisha ubora wa taaluma kwa kuhakikisha wahitimu wake wanakuwa na ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira ndani na nje ya nchi. “Tunataka mkitoka hapa muwe na ujuzi, siyo vyeti tu. Mzumbe inawapa uwezo wa kutatua matatizo, kufanya kazi kwa tija na kujisimamia. Hadhi ya Chuo hiki ipo mikononi mwenu,” alisema Prof. Mwegoha huku akihimiza wanafunzi kuwa mabalozi wa chapa ya Mzumbe. Ameeleza pia kuwa Chuo kinaendelea na maboresho ya miundombinu, ikiwemo ukarabati wa madarasa na uwekaji wa taa za sola katika viwanja vya michezo ili viweze kutumika hata nyakati za jioni. Pia, katika kikao hicho, Prof. Mwegoha alimtambulisha rasmi Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui Petro. Akizungumza na wanafunzi hao Prof. Tundui amesisitiza wanafunzi kufuata miongozo ya kitaaluma ya Chuo ikiwa ni pamoja na kujisajili mapema kabla ya mitihani, kushiriki kikamilifu katika masomo na kujenga nidhamu binafsi. Pia, Prof. Tundui alihimiza matumizi sahihi ya teknolojia ya Akili Mnemba (AI). “Akili Mnemba (AI) iwe nyenzo ya kuwasaidia kuelewa zaidi, si kubandika majibu bila kufahamu. AI iwe rafiki yako wa kumuuliza maswali, si mbadala wa wewe kufikiri,” amesisitiza Prof. Tundui. Aidha, aliwahimiza wanafunzi kutumia maktaba kwa ufanisi na kujijengea umahiri kama vile uwasilishaji wa hoja, kujiamini na mawasiliano bora, ili kujiandaa vyema kwa ushindani katika soko la ajira. Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Fedha, Mipango na Utawala, Prof. Allen Mushi, alieleza kuhusu miradi mbalimbali ya ukarabati iliyokamilika na inayoendelea chuoni, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu na huduma kwa wanafunzi. Alisisitiza kuwa jitihada hizo zinafanywa kwa manufaa ya wanafunzi wote, hivyo kila mmoja anapaswa kuwa na moyo wa uzalendo kwa kuitunza miundombinu hiyo. “Tunafanya haya yote kwa ajili yenu. Ukiona sehemu yoyote inahitaji marekebisho, toa taarifa mapema. Usikubali kuwa sehemu ya uharibifu,” alisisitiza Prof. Mushi. Wanafunzi walipata nafasi ya kutoa hoja, kuuliza maswali na kutoa mapendekezo mbalimbali. Masuala yaliyoibuliwa ni pamoja na uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA, upatikanaji wa vitabu katika maktaba, changamoto za usajili wa kozi pamoja na uhitaji wa nafasi zaidi za kujisomea. Uongozi wa Chuo uliahidi kuendelea kujenga utamaduni wa kusikiliza na kushirikiana na wanafunzi kupitia majukwaa mbalimbali kama vile School Baraza, linalowakutanisha viongozi wa wanafunzi na Wakuu wa Skuli na Ndaki, kwa ajili ya kushughulikia hoja na kuboresha huduma chuoni.