News-Details

News >Details

WANAFUNZI NDAKI YA MBEYA WAELEZWA FURSA KATIKA MATUMIZI YA JUKWAA LA KIDIGITALI LA M-WEKEZA

WANAFUNZI NDAKI YA MBEYA WAELEZWA FURSA KATIKA MATUMIZI YA JUKWAA LA KIDIGITALI LA M-WEKEZA

Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya, kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania, kimeendesha Mhadhara kwa Umma tarehe 31 Mei, 2025 uliojikita katika kujadili masuala ya uwekezaji kidigitali na elimu ya fedha kwa maendeleo ya wanafunzi wa vyuo vikuu. Mada kuu ya mhadhara huo ilikuwa “Ufunguaji wa Fursa kwa Vijana (Wanafunzi wa Vyuo Vikuu) Kupitia Jukwaa la Kidigitali la M-WEKEZA.” Akifungua mhadhara huo, Kaimu Rasi wa Ndaki ya Mbeya, Dkt. Kennedy Makafu, alisisitiza umuhimu wa wanafunzi kusikiliza kwa makini mada zitakazowasilishwa. Pia, aliwapongeza waandaji wa tukio hilo na kutoa rai ya kufanyika kwa mihadhara ya umma mara kwa mara chuoni ili kuhamasisha vijana kutafuta fursa za kuleta maendeleo. Naye Bw. Sylvester Luleka, Mtaalamu wa Fedha Kidigitali, alitoa ufafanuzi kuhusu jukwaa la kidigitali la M-WEKEZA na kueleza fursa zilizopo ndani ya jukwaa hilo. Alieleza kuwa jukwaa hilo linamwezesha kijana kuwekeza fedha kidigitali na, mara atakapo hitimu masomo yake, kutumia fedha hizo kuongeza kipato na kujiajiri, jambo ambalo litamsaidia kushinda changamoto ya ajira nchini. Vilevile, wanafunzi walipewa elimu kuhusu nidhamu ya fedha na jinsi ya kupanga bajeti kwa fedha walizonazo. Washiriki wa mhadhara huo walipata fursa ya kuuliza maswali na kutoa maoni yao. Wengi walihitaji kufahamu changamoto zinazokumba matumizi ya jukwaa la M-WEKEZA. Wengine walisisitiza kuwa kwa kuwa ujuzi wa kutumia majukwaa ya kidigitali kutafuta fursa bado ni mdogo, basi elimu ya aina hiyo iendelezwe zaidi kwa njia ya makongamano, mihadhara, na bonanza. Mhadhara huo uliofanyika Ndaki ya Mbeya ulionekana kufanikisha malengo yake, kwani vijana wengi waliohudhuria walionesha ari kubwa ya kujifunza zaidi kuhusu uwekezaji na fursa zake. Chuo Kikuu Mzumbe kinaalika wadau wote wa maendeleo kushirikiana kuandaa na kuendesha mihadhara kama hii, ambayo inalenga kutoa ujuzi na maarifa kwa vijana wetu ili kuchochea maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.

None
None
None
None
None
None
None
None