News-Details

News >Details

CHUO KIKUU MZUMBE CHAWANOA WANAFUNZI WA SEKONDARI YA KIJITONYAMA KATIKA MATUMIZI YA MAKTABA

CHUO KIKUU MZUMBE CHAWANOA WANAFUNZI WA SEKONDARI YA KIJITONYAMA KATIKA MATUMIZI YA MAKTABA

Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki yake ya Dar es Salaam, tarehe 3 Juni, 2025 kimeendesha mafunzo kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kijitonyama Sayansi iliyopo Kata ya Kijitonyama, Wilaya ya Kinondoni kuhusu matumizi sahihi ya maktaba na maktaba mtandao ikiwa ni sehemu ya jitihada za taasisi hiyo kushiriki katika utoaji wa huduma kwa jamii. Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkuu wa Kitengo Cha Maktaba Ndaki ya Dar es Salaam, Bw. Elias Ntobi alisema kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha wanafunzi kuelewa aina mbalimbali za maktaba na namna bora ya kuzitumia katika kujifunza. Alisisitiza kuwa maktaba mtandao ni nyenzo muhimu inayorahisisha upatikanaji wa taarifa kwa kutumia vifaa vya kielektroniki kama simu janja na kompyuta. Aidha, Bw. Ntobi aliwahimiza wanafunzi kuendeleza tabia ya kujisomea (reading habit), akieleza kuwa kuwa na utamaduni wa kusoma si tu kunaboresha matokeo ya masomo bali pia huchangia kufanya maamuzi sahihi katika maisha ya kila siku na kuongeza kuwa jamii iliyo na taarifa sahihi ni jamii iliyostaarabika. Kwa upande wake, Afisa Maktaba Msaidizi, Bw. Benard Msengi alieleza kuwa maktaba mtandao huwapa wanafunzi fursa ya kujifunza kutoka mahali popote bila kulazimika kufika kwenye jengo la maktaba kwa kutumia viunganishi mbalimbali wanavyoweza kupata taarifa za masomo. Aidha, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kijitonyama Sayansi, Bi. Rukia Butenge, alikipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kutoa elimu hiyo muhimu kwa wanafunzi kwani wamejifunza mambo mapya ambayo hapo awali hatukuyafahamu vizuri. "Wanafunzi wetu sasa wanaweza kujifunza kwa njia ya kujitegemea hata bila uangalizi wa karibu kutoka kwa walimu popote walipo”. Alisisitiza Mwl. Butenge Mkutubi Msaidizi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Bw. Fred Kivike, aliwafahamisha wanafunzi hao kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo na kuwakaribisha kujiunga na chuo hicho pindi watakapomaliza elimu yao ya sekondari. Chuo Kikuu Mzumbe kimekuwa kikitekeleza Mpango Mkakati wa kurudisha huduma kwa jamii kama sehemu ya majukumu ya msingi ya uelimishaji na kujenga jamii yenye maarifa.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None