Chuo Kikuu Mzumbe kimeadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, Juni 5, 2025 kwa njia ya kipekee kwa kutoa elimu ya udhibiti wa taka za plastiki kupitia shughuli mbalimbali za kimazingira zilizofanyika katika Kampasi Kuu ya Chuo hicho, Morogoro. Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Klabu ya Wanafunzi ya Kutunza Mazingira ya Chuo Kikuu Mzumbe, inayolelewa na Idara ya Usimamizi wa Mazingira chini ya Taasisi ya Masomo ya Taaluma za Maendeleo, yalibeba kaulimbiu: Mazingira yetu na Tanzania Ijayo, Tuwajibike sasa kudhibiti matumizi ya plastiki. Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mgeni Rasmi katika tukio hilo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi alieleza kuwa elimu ya mazingira ni msingi wa mabadiliko ya tabia na mtazamo wa jamii katika kulinda rasilimali za asili. “Tunahitaji kuchukua hatua sasa kabla madhara hayajawa makubwa zaidi. Udhibiti wa taka hususani plastiki, ni wajibu wa kila mmoja wetu. Chuo chetu kinaendelea kujitoa kwa vitendo katika kulinda mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Prof. Mushi. Kwa upande wake, Afisa Afya – Mazingira wa Chuo Kikuu Mzumbe, Bw. Casto Semiono, alieleza kuwa taka za plastiki huchukua muda mrefu kuoza na husababisha athari kubwa katika mazingira. Aliongeza kuwa hatua za kielimu na za kimkakati zinahitajika ili kuhamasisha matumizi ya bidhaa mbadala na Uchakataji upya wa plastiki. Naye Rais wa Klabu ya Wanafunzi ya Mazingira Chuo Kikuu Mzumbe, Bw. Philipo Kisizi, alisema kuwa wanafunzi wamekuwa mstari wa mbele katika kushiriki shughuli za uhifadhi wa mazingira kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kampeni za usafi, upandaji miti na utoaji elimu kwa jamii. “Kama vijana, tunatambua wajibu wetu katika kujenga Tanzania endelevu. Tunaamini kuwa mabadiliko makubwa huanzia na hatua ndogo tunazochukua kila siku,” alisema Kisizi. Katika kuonyesha dhamira thabiti ya kulinda mazingira, washiriki wa maadhimisho hayo wakiwemo wanafunzi, watumishi na viongozi wa chuo wakiongozwa na mgeni rasmi, walishiriki kwa pamoja katika zoezi la kukusanya taka za plastiki maeneo mbalimbali ya chuo kama ishara ya msisitizo wa udhibiti wa taka hizo. Chuo Kikuu Mzumbe kimejipambanua kuwa taasisi ya elimu inayozingatia maendeleo endelevu kwa vitendo, kwa kutoa elimu inayojikita si tu kwenye nadharia, bali pia katika kushughulikia changamoto halisi za kijamii, kiuchumi na kimazingira.