Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, kimeandaa Mhadhara wa Umma uliohusu Simulizi kwa ajili ya Kubadili Maisha katika Jamii "Story Telling for Social Change". Mhadhara huo ulilenga kuwasaidia kuwa wabunifu, kuanzisha taasisi, pamoja na kuwa na mawazo mbadala ya kusaidia jamii kukabiliana na changamoto mbalimbali. Akizungumza Juni 6, 2025, Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es salaam (Kituo cha Tegeta), Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo ya Kozi za Muda Mfupi, Ubunifu na Ushauri wa Kitaalamu Dkt. Darlene Mutalemwa, amesema lengo kuu la mhadhara huo ni kuongeza uelewa kwa wanafunzi namna ya kupata uzoefu wa kitaaluma unaowasaidia kufikia ndoto zao na kusaidia jamii. Kwa upande wake, Mtoa Mada katika mhadhara huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya TAI inayojihusisha na utoaji wa elimu kwa jamii, Bw. Ian Tarimo, amesema wanafunzi hao wamepata uzoefu wa namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakumba wananchi katika maeneo yao ikiwemo kupinga mila na desturi potofu pamoja na elimu ya mabadiliko ya tabia nchini. Aidha, Bw. Tarimo amekipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuanzisha programu zinazowajengea wanafunzi uwezo wa vitendo, ikiwemo kuwaunganisha na sekta binafsi ili kupata uzoefu kwa kuunganisha elimu ya darasani na uzoefu wa vitendo ambao utaimarisha ujuzi na weledi utakaowasaidia kuchangia maendeleo ya Taifa. "Mafunzo haya ya simulizi yanawajengea wanafunzi uwezo wa kuchambua mambo kwa undani katika jamii na kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za kijamii, jambo ambalo lina tija kwa Taifa," amesema Bw. Tarimo. Naye, Mhadhiri Msaidizi kutoka Ndaki ya Dar es Salaam - Idara ya Sayansi ya Jamii na Insia, Bw. Emmanuel Komba, amesema kuwa mhadhara huo ni rafiki kwa wanafunzi kwani wameweza kupata maarifa bora. Alisema kuwa wao kama walimu wanaendelea kuunga mkono jitihada za Chuo za kuhakikisha wahitimu wanaozalishwa na Chuo hicho wana uwezo mkubwa wa kuchangia maendeleo ya Taifa. Kwa upande wao, wanafunzi walioshiriki mhadhara huo wakiwemo Joseph Magoti na Suzan Methusela, wanaosoma Shahada ya Utawala wa Umma, wameushukuru uongozi wa Chuo kwa kuandaa mihadhara.