News-Details

News >Details

NDAKI YA MBEYA YAZINDUA RASMI KLABU YA MILIKI BUNIFU

NDAKI YA MBEYA YAZINDUA RASMI KLABU YA MILIKI BUNIFU

Kupitia Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Chuo Kikuu Mzumbe na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Ndaki ya Mbeya imezindua rasmi Klabu ya Miliki Bunifu tarehe 6 Juni 2025. Klabu hiyo ni ya kwanza ya aina yake kuzinduliwa nchini Tanzania. Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wanafunzi, wahadhiri pamoja na wawakilishi kutoka BRELA, Vodacom, na Benki Kuu ya Tanzania. Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Rasi wa Ndaki ya Mbeya, Prof. Charles Tundui, alieleza kuwa uzinduzi wa klabu hiyo utapanua wigo wa ushirikiano kati ya chuo na wadau mbalimbali katika nyanja za elimu, ubunifu, na tafiti. Naye, Mkurugenzi wa Miliki Bunifu kutoka BRELA, Bi. Loy Mhando ambaye alikuwa Mgeni rasmi wa tukio hilo, alibainisha kuwa Chuo Kikuu Mzumbe – Ndaki ya Mbeya ni taasisi ya kwanza nchini kuzindua Klabu ya Miliki Bunifu. Alisisitiza kuwa BRELA ipo tayari kushirikiana na klabu hiyo katika kutoa elimu, kuhamasisha na kukuza uelewa wa masuala ya miliki bunifu kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Miongoni mwa matukio muhimu katika hafla hiyo yalikuwa ni uzinduzi wa katiba rasmi ya klabu, utambulisho wa nembo (logo) ya klabu, pamoja na kuapishwa kwa viongozi wapya wa klabu hiyo. Hatua hizi zinalenga kuimarisha misingi ya uongozi bora, uwazi na uwajibikaji ndani ya klabu. Mlezi na mshauri wa klabu hiyo, Dkt. Kennedy Makafu, alieleza kuwa lengo kuu la klabu ni kuwajengea wanafunzi uelewa wa kina juu ya umuhimu wa kulinda bunifu zao, sambamba na kuwapatia mwongozo wa kitaalamu na kisheria. Aliwahimiza wanafunzi ambao bado hawajajiunga na klabu hiyo kufanya hivyo mapema ili kunufaika na fursa zilizopo. Kwa ujumla, uzinduzi huo umeonekana kuwa hatua muhimu katika kuimarisha ubunifu, ulinzi wa haki miliki, na kuchochea ujasiriamali miongoni mwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe – Ndaki ya Mbeya.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None