Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amekutana na Watumishi wa Ndaki ya Dar es Salaam tarehe 9 Juni 2025 katika kikao maalumu kilicholenga kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya chuo na ustawi wa watumishi. Akizungumza katika kikao hicho, Prof. Mwegoha aligusia masuala yanayohusu hali ya watumishi na chuo kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na ongezeko la idadi ya watumishi ambayo imefikia 104 katika Ndaki hiyo. Aidha, Akiwa kama mlezi wa mfuko wa faraja Chuo Kikuu Mzumbe, alisisitiza kuwa ni chombo muhimu kwa ustawi wa watumishi na hivyo ni muhimu kuongeza ushiriki. Aliongeza kuwa kila mtumishi ana jukumu la kulinda taswira ya chuo, akisisitiza kuwa hadhi ya Chuo Kikuu Mzumbe ni kubwa na kila mmoja anapaswa kuwa sehemu ya kuitunza kupitia uwajibikaji na ufanisi wa kazi. Alisisitiza kuwa wanataaluma na watumishi wa upande wa utawala wote wanapaswa kushirikiana kwa karibu katika kutekeleza majukumu ya taasisi. Alihimiza mshikamano na kazi kwa pamoja, akisema “Teamwork is our mission.” Pia, alieleza kuwa chuo kinaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Kampasi ya Tanga kupitia Mradi wa HEET, ukarabati wa barabara za ndani na miundombinu katika kampasi zote, ukarabati wa jengo la kihistoria la Lumumba pamoja na nyumba za watumishi na kuendeleza mafunzo na maendeleo ya rasilimali watu. Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui, alisisitiza umuhimu wa kila mtumishi kuwajibika katika nafasi yake ili kuhakikisha ubora wa huduma na utoaji wa elimu. Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi, alieleza kuwa chuo kinaendelea na maandalizi ya Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Sita (Corporate Strategic Plan), na kuwataka watumishi kushiriki kikamilifu kwa kutoa maoni, mapendekezo na ushauri ili kuhakikisha mpango huo unakidhi mahitaji halisi ya taasisi. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu, Bi. Sophia Mchomvu, alisisitiza umuhimu wa watumishi kuhakikisha taarifa zao katika mfumo wa PEPMIS zinawasilishwa na kutumwa ipasavyo. Alieleza kuwa uongozi si jina tu, bali unahitaji kuwa na moyo wa kuwajali wanaoongozwa kwa kuhakikisha wanapewa mwongozo na nafasi ya kukua kitaaluma na kikazi. Kikao hiki kilikuwa jukwaa muhimu kwa watumishi kutoa maoni yao na kupata mwelekeo kutoka kwa uongozi wa juu wa chuo kuhusu maendeleo na mustakabali wa taasisi.