News-Details

News >Details

MZUMBE KUANZISHA STASHAHADA YA UMAHIRI YA UBUNIFU WA KIJAMII NA UJASIRIAMALI KUPITIA MRADI WA ADVANCE

MZUMBE KUANZISHA STASHAHADA YA UMAHIRI YA UBUNIFU WA KIJAMII NA UJASIRIAMALI KUPITIA MRADI WA ADVANCE

Chuo Kikuu Mzumbe kimeanza mchakato wa kuanzisha Stashahada ya Umahiri ya Ubunifu wa Kijamii na Ujasiriamali kupitia Mradi wa ADVANCE (Advancing Social Innovation and Entrepreneurship through Postgraduate Education in East Africa). Warsha ya wadau wa mradi huo imefanyika leo tarehe 12 Juni 2025 katika Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro na kufunguliwa rasmi na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui. Warsha hiyo imelenga kupitia na kuandaa mtaala wa programu hiyo ya mwaka mmoja, itakayofundishwa kwa mfumo mseto wa ujifunzaji (blended learning), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwajengea wahitimu ujuzi wa kutatua changamoto halisi za kijamii kwa njia bunifu na jumuishi. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Prof. Tundui alibainisha kuwa soko la ajira kwa sasa linahitaji wataalamu wenye uwezo wa vitendo, ubunifu na mawazo mapya. Aliwataka wadau kushiriki kikamilifu katika mjadala wa uboreshaji wa mtaala huo ili kuhakikisha unakidhi mahitaji halisi ya jamii na uchumi wa sasa. “Nawapongeza waandaaji wa mradi na washiriki wote kwa kufanikisha hatua hii muhimu. Tunahitaji mtaala unaojibu mahitaji ya sasa ya kijamii kwa kutumia njia bunifu na zenye tija,” alisema Prof. Tundui. Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa ADVANCE kwa upande wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Jenifer Sessabo, aliuelezea mradi huo kuwa ni ushirikiano wa kimataifa kati ya nchi za Tanzania, Uganda, Italia na Bulgaria, ukihusisha jumla ya washirika 10. Alifafanua kuwa mradi huu unalenga kukuza ubunifu wa kijamii na ujasiriamali kwa kuanzisha programu maalumu ya stashahada ya umahiri katika vyuo vikuu vinne kutoka nchi hizo. Prof. Sessabo alieleza kuwa mradi huu utakuwa chachu ya mabadiliko kwa Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuchochea uboreshaji wa mitaala, kukuza ushirikiano kati ya chuo na jamii, kuimarisha mitandao ya kimataifa, na kuongeza mwelekeo wa kijasiriamali miongoni mwa wanafunzi na wahadhiri. “Mtaala tunaoandaa utawezesha wanafunzi kupata maarifa na ujuzi wa kuibua suluhisho bunifu kwa changamoto za kijamii, jambo ambalo ni muhimu sana kwa maendeleo endelevu,” alisisitiza Prof. Sessabo. Katika warsha hiyo, Dkt. Mushumbusi Kato, ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe, aliendesha mafunzo kuhusu dhana ya ubunifu wa kijamii na ujasiriamali (Social Innovation and Entrepreneurship - SIE) na kueleza sifa muhimu zinazomtofautisha mjasiriamali bunifu wa kijamii, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kuona fursa ndani ya changamoto na kuchukua hatua zenye kuleta mabadiliko chanya kwa jamii. Warsha hii imekuwa jukwaa muhimu kwa wadau kujadili kwa kina namna ya kuunda mtaala madhubuti na unaoendana na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, kwa lengo la kutoa elimu yenye tija na athari chanya katika jamii.

None
None
None
None
None
None
None
None
None