Ndaki ya Mbeya ilipata heshima kubwa ya kupokea ujumbe maalumu kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), tarehe 13 Juni 2025. Ziara hiyo ililenga kuimarisha ushirikiano kati ya chuo na UNDP katika nyanja za maendeleo endelevu, ubunifu, na kuwajengea uwezo watumishi pamoja na wanafunzi. Ujumbe huo uliongozwa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Shigeki Komutsabara, na kupokelewa rasmi na uongozi wa chuo ukiongozwa na Rasi wa Ndaki ya Mbeya, Prof. Henry Mollel. Akizungumza katika ziara hiyo, Rasi wa Ndaki ya Mbeya, Prof. Henry Mollel aliipongeza UNDP kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya vijana nchini na kuonesha utayari wa Chuo Kikuu Mzumbe kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya wanafunzi na jamii kwa ujumla. Kwa upande wao, UNDP walivutiwa na juhudi za chuo katika kukuza ubunifu na uendelevu wa mazingira, na walieleza nia yao ya kusaidia vijana katika nyanja za uongozi bora, vipaji, ili kuleta mabadiliko chanya kwa vijana. Ziara hiyo ilihitimishwa kwa kutembelea maeneo mbalimbali ya chuoni hapo kama vile madarasa, maktaba, kumbi za mikutano, hosteli za wanafunzi, kituo cha afya na ofisi za watumishi. Katika mazungumzo yao, pande zote mbili zilijadili fursa za kushirikiana katika miradi ya kijamii, tafiti za kisayansi, na programu za ujasiriamali kwa wanafunzi.