Wanataaluma wa Kitivo cha Sayansi za Jamii katika Chuo Kikuu Mzumbe wamepatiwa mafunzo ya siku moja kuhusu uandishi wa mapendekezo yanayoweza kushinda ufadhili wa miradi ya utafiti pamoja na ufadhili wa kutekeleza miradi isiyo ya kuutafiti. Vilevile, wanataaluma hao walipata kuelezwa umuhimu wa afya na ujumuishaji wa anuai za kijamii katika mazingira ya kazi. Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 14 Juni 2025, katika Kampasi Kuu ya Chuo hicho – Morogoro (Eneo la Maekani). Akifungua mafunzo hayo, Mtiva wa Kitivo hicho, Dkt. Harold Utouh aliwataka wanataaluma kuyachukulia kwa uzito mafunzo hayo kwa kuwa yana mchango mkubwa katika kuongeza ushindani wa maandiko yao ya miradi, hivyo kusaidia upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali. Mwezeshaji Mkuu wa mafunzo hayo, Prof. Mackfallen Anasel kutoka Skuli ya Utawala wa Umma na Menejimenti (SoPAM) Chuo Kikuu Mzumbe, alibainisha kuwa miradi inayopaswa kuandaliwa inajumuisha tafiti za kitaaluma, miradi ya utekelezaji wa huduma au teknolojia, mafunzo ya kujengea jamii uwezo, ushiriki wa makongamano ya kitaaluma, msaada wa vifaa, na ufadhili wa mwanzo kwa tafiti mpya. Pia, alieleza kuwa andiko bora linapaswa kuwa na vipengele muhimu kama kichwa cha mradi kichomvutia kinachoelweka kirahisi na chenye mvuto, historia ya changamoto iliyoelezwa vema, malengo mahsusi, mbinu za utafiti zinazoonesha ni namna gani nzuri mradi utatekelezwa, bajeti yenye uhalisia, ratiba ya utekelezaji inayoendana vema na taarifa nyingine katika pendekezo, matokeo yanayotarajiwa, na mpango wa uendelevu wa mradi. Vilevile, alitoa tahadhari kuhusu makosa ya kawaida kama malengo yasiyoeleweka, bajeti zisizo na uhalisia, matarajio makubwa kupita kiasi, uandishi usio na mpangilio mzuri na ukosefu wa ubunifu. Kwa wanataaluma wachanga, alihimiza ushiriki kwenye timu za utafiti, warsha, na makongamano; kujisajili kwenye mitandao ya taarifa za ufadhili wa miradi; kushirikiana na wataalamu waliobobea; na kuanza kujenga wasifu wa kitaaluma mapema. Naye Mratibu wa Elimisha Rika wa Kitivo hicho, Dkt. Martina Duwe alisisitiza umuhimu wa kujenga mazingira ya kazi yanayojumuisha anuai za kijamii kama vile tofauti za umri, hali ya ulemavu na jinsi. Alikumbusha kuwa afya bora kwa watumishi, hasa wanaoishi na VVU/UKIMWI, ni msingi wa utendaji kazi wenye tija. Kwa upande wake, Dkt. Athuman Malendemla kutoka Kitengo cha Huduma za Tiba na Uangalizi katika Kituo cha Afya Mzumbe, aliwapa wanataaluma elimu kuhusu kifaa cha OraQuick kinachowezesha mtu kujipima VVU kwa kutumia mate, kwa usiri na urahisi. Alisema kifaa hicho ni njia bora ya kuongeza mwitikio wa upimaji wa hiari na utambuzi wa mapema wa hali ya afya.