News-Details

News >Details

MZUMBE YAJIPAMBANUA KATIKA MASHINDANO YA MDAHALO YA AFRIKA MASHARIKI NA MAREKANI

MZUMBE YAJIPAMBANUA KATIKA MASHINDANO YA MDAHALO YA AFRIKA MASHARIKI NA MAREKANI

Chuo Kikuu Mzumbe kinashiriki katika mashindano ya kimataifa ya mdahalo yajulikanayo kama Social Justice Debate Arusha ambayo yanalenga kujadili masuala ya haki ya kijamii katika muktadha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mashindano hayo yameanza tarehe 14 Juni 2025 na yanatarajiwa kufikia tamati tarehe 15 Juni 2025, yakifanyika jijini Arusha, Tanzania kwa lengo la kujadili na kuchambua mada isemayo “Mfumo wa Uhamiaji wa Haki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanikiwa vizuri zaidi kupitia utekelezaji kamili wa Itifaki ya Soko la Mitaji badala ya kuweka kipaumbele katika hatua za kuajiri.” Kwa mujibu wa Mratibu wa Mazoezi ya Mahakama ya Mfano na Kituo cha Msaada wa Kisheria kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Wakili Bernadetha Iteba, mashindano hayo yamekusanya vyuo mbalimbali kutoka nchi za Afrika Mashariki pamoja na Marekani, yakilenga kukuza uwezo wa wanafunzi katika kujenga hoja, mijadala ya kisheria na uongozi wa kimataifa. Timu ya Chuo Kikuu Mzumbe inayoshiriki mdahalo huu imeundwa na wanafunzi sita ambao ni Sakina Kasabe, Thabitha Ndabile, Reuben Charles, Charles Mjanasa, Reuben King na Godfrey Gama. Wanafunzi hao wanaongozwa na wakufunzi wao ambao pia ni wahadhiri wasaidizi Deogratias Mapendo, Peter Kipfumu na Immaculate Batulaine. Mashindano haya yanachukuliwa kuwa fursa muhimu kwa Chuo Kikuu Mzumbe kuonesha umahiri wa wanafunzi wake katika nyanja ya sheria na haki ya kijamii, sambamba na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa kupitia mijadala ya kisomi.

None