News-Details

News >Details

MZUMBE – NDAKI YA DAR ES SALAAM YATUMIA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA KUTOA ELIMU YA UWEKEZAJI NA USAWA WA JINSIA

MZUMBE – NDAKI YA DAR ES SALAAM YATUMIA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA KUTOA ELIMU YA UWEKEZAJI NA USAWA WA JINSIA

Katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2025, Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam kimeendesha mafunzo mahsusi kwa watumishi wake kuhusu uwekezaji na usawa wa kijinsia, yakiwa na lengo la kuboresha ufanisi kazini na maandalizi ya maisha baada ya kustaafu. Akifungua rasmi maadhimisho hayo Juni 17, 2025, Naibu Rasi wa Ndaki hiyo, Prof. Omary Swalehe, aliwataka watumishi kuwa na uelewa wa kina wa taratibu na miongozo ya kiutumishi kwa kutembelea Ofisi za Rasilimali Watu na Huduma za Kitawala, ili kuongeza uwajibikaji na tija katika kazi zao. Prof. Swalehe alieleza kuwa mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za Chuo katika kuhakikisha watumishi wake wanajiandaa mapema kwa maisha ya kustaafu kwa amani na heshima, pamoja na kuimarisha usawa wa kijinsia katika jamii. Aidha, Mkuu wa Idara ya Masomo ya Biashara, Dkt. Joshua Mwakujonga aliwasilisha mada ya uwekezaji na ujasiriamali, akisisitiza umuhimu wa watumishi kuwa wabunifu, kupanga na kutumia muda kwa ufanisi ili kufanikisha malengo yao ya kifedha. Naye Mratibu wa Taifa wa Jukwaa la Walimu Wanawake Bara la Afrika nchini Tanzania (FAWE-Tanzania), Bi. Neema Kitundu aliwasilisha mada kuhusu usawa wa kijinsia na kuhimiza kuzingatia haki sawa katika familia, kazi na jamii, akieleza kuwa usawa huo ni kichocheo cha maendeleo ya taifa. Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo cha Tegeta na Dawati la Jinsia, Dkt. Janeth Patrick Swai aliushukuru uongozi wa Chuo kwa kuandaa mafunzo yenye tija, akisema yamewasaidia watumishi kutafakari namna bora ya kujenga maisha yenye usawa, ufanisi na maandalizi ya kustaafu. Maadhimisho haya yaliendeshwa kwa kaulimbiu: “Himiza Matumizi ya Kidigitali ili kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchangia Uwajibikaji.”

None
None
None
None
None
None
None
None
None