Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Umoja wa Wanataaluma Chuo Kikuu Mzumbe (MUASA), kwa udhamini wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), kimeendesha Mhadhara wa Umma tarehe 4 Juni 2025 katika Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro, uliolenga kujadili “Uchambuzi wa changamoto za kisheria zinazowakabili wanawake wanaoishi na wanaume bila ndoa rasmi baada ya mahusiano kuvunjika nchini Tanzania (Bara).” Mhadhara huo umehudhuriwa na wanataaluma pamoja na wanafunzi kutoka vitivo mbalimbali vya Chuo Kikuu hicho. Akiwasilisha mada hiyo, Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Profesa Cyriacus Binamungu, alieleza kuwa licha ya wanawake wengi kuishi na wanaume kwa miaka mingi kama mume na mke, hali hiyo haiwapi kinga yoyote ya kisheria iwapo uhusiano huo utakoma. “Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 haikupi ulinzi iwapo haupo kwenye ndoa rasmi – iwe ya kimila, kidini au ya kiserikali. Wanawake wengi huishia kunyimwa haki za msingi kama mgawanyo wa mali, matunzo ya watoto, na fidia ya kiuchumi wanapoachwa,” alisema Prof. Binamungu. Aliongeza kuwa kuna ombwe kubwa la kisheria linalosababisha wanawake wengi kuathirika kisaikolojia, kijamii na kiuchumi, licha ya kuwa walikuwa sehemu ya ujenzi wa familia kwa muda mrefu. Aidha, Mada hiyo ilichambuliwa kwa kina na Mhadhiri wa Sheria kutoka Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Lukiko Lukiko, ambaye alisisitiza kuwa hali hiyo inatokana na tafsiri finyu ya sheria zilizopo. “Sheria za Tanzania bado hazitambui hadhi ya mahusiano yasiyo rasmi kama ndoa. Hili linawaweka wanawake wengi kwenye mazingira ya kutopata haki zao, hata pale ambapo ushahidi wa mchango wao kwenye familia upo wazi,” alisema Dkt. Lukiko. Baada ya uwasilishaji na uchambuzi wa mada, washiriki wa mhadhara huo walipewa nafasi ya kumuuliza maswali Prof. Binamungu, ambapo maswali mengi yalihusu tafsiri ya uchumba wa muda mrefu bila ndoa rasmi (cohabitation) na uwezekano wa Tanzania kuiga mifumo ya nchi nyingine zinazotambua kisheria hali hiyo. Akijibu hoja hizo, Prof. Binamungu alisema: “Ni kweli baadhi ya nchi zinaruhusu kutambua ‘common law marriage’, lakini kwa Tanzania bado hakuna msingi wa kisheria unaotoa ulinzi huo.” Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kuwa kielelezo cha taasisi inayotanguliza mijadala ya kitaaluma kwa ajili ya ustawi wa jamii na maendeleo ya sheria nchini. Kupitia Mhadhara huu wa Umma, kimeonesha umuhimu wa kujadili kwa kina hatma ya wanawake walioko katika mahusiano yasiyo rasmi, hasa kwa kuzingatia haki zao za kisheria.