Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe limevutiwa na kupongeza hatua za utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Kampasi mpya katika Wilaya ya Mkinga, Jijini Tanga. Hatua hii ni baada ya kufanya ziara maalumu iliyofanyka Julai 1, 2025. Ziara hiyo iliyoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Baraza, CPA Pius Maneno imelenga kufuatilia na kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) chuoni hapo. Mbali na Wajumbe wa Baraza, ziara hiyo imehusisha baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Chuo, Waratibu wa Mradi wa HEET, Timu ya Usimamizi wa Mradi kwa upande wa Mkandarasi ‘Dimetoclasa Real Hope Ltd’ na Mshauri Elekezi ‘Mekon Arch. Consultant Ltd’. Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, CPA Maneno ameipongeza timu nzima kwa weledi na usimamizi madhubuti wa mradi huo, akisisitiza kuwa Baraza linaendelea kufuatilia kwa karibu kuhakikisha thamani ya fedha za umma inaonekana kwa ubora na viwango stahiki. “Ni faraja kuona mradi unatekelezwa kwa kasi na ubora unaotakiwa. Baraza litaendelea kuwa bega kwa bega hadi mwisho,” alisema CPA Maneno. Awali, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha aliwasilisha taarifa kwa Wajumbe wa Baraza akibainisha hatua zilizofikiwa, mafanikio na changamoto zinazoshughulikiwa kwa ushirikiano na wadau. Alisisitiza kuwa mradi huu ni kichocheo muhimu cha upanuzi wa fursa za elimu ya juu nchini. Kwa upande wake Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET, Dkt. Lihoya Chamwali alieleza kuwa utekelezaji umefikia wastani wa asilimia 57.5, huku hosteli za wanafunzi zikiwa zimefikia asilimia 58, nyumba za watumishi asilimia 68, jengo la taaluma asilimia 57, bwalo la chakula asilimia 56 na kituo cha afya asilimia 58. Wajumbe wa Baraza na wageni walipata fursa ya kukagua hatua ya ujenzi na kuridhishwa na kasi na ubunifu wa usanifu. Waliwasihi wakandarasi kuendelea kudumisha ubora na kukamilisha kazi kwa muda uliopangwa ili kuhakikisha vijana wa Kitanzania wananufaika na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.