News-Details

News >Details

MZUMBE YAWEZESHA TAASISI ZA WIZARA YA NISHATI KUPITIA MAFUNZO YA UFUATILIAJI NA TATHMINI JIJINI DODOMA

MZUMBE YAWEZESHA TAASISI ZA WIZARA YA NISHATI KUPITIA MAFUNZO YA UFUATILIAJI NA TATHMINI JIJINI DODOMA

Kituo cha Umahiri cha Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, kikiongozwa na Profesa Mackfallen Anasel, kimeendesha mafunzo ya siku tano kwa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati, kuhusu masuala ya Ufuatiliaji na Tathmini, yaliyofanyika jijini Dodoma kuanzia tarehe 23 hadi 27 Juni, 2025. Lengo kuu la mafunzo haya lilikuwa ni kuzijengea uwezo taasisi hizo ili ziweze kuboresha kwa ufanisi zaidi utendaji wao wa kazi, kufuatilia utekelezaji wa miradi, pamoja na kufanya tathmini ya kimkakati katika shughuli zao za kila siku. Taasisi zilizoshiriki katika mafunzo haya ni pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), na Kampuni ya Ujenzi na Matengenezo ya Usambazaji na Usafirishaji wa Umeme (ETDCO). Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Nishati, Bi. Anitha R. Ishengoma, alisisitiza kuwa ufuatiliaji na tathmini ni nyenzo muhimu ya kusimamia matumizi bora ya rasilimali, kuhakikisha uwajibikaji, na kufikia malengo ya maendeleo ya kitaifa. “Ufuatiliaji na tathmini ni kama kioo cha shirika – kinachoonesha hali halisi ya utendaji na mafanikio ya kazi zetu,” alieleza. Kwa upande wake, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, aliwahimiza washiriki kutumia maarifa waliyopata kuboresha utendaji, uwajibikaji na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi katika taasisi zao. “Mafunzo haya yaweni kichocheo cha kimkakati katika kuboresha miradi ya sekta ya nishati. Wizara itaendelea kuwajengea uwezo wataalam wake kupitia mafunzo ya mara kwa mara,” alisema Mhandisi Luoga. Aidha, Mhandisi Luoga alikipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kutoa mafunzo hayo, na kusisitiza kuwa athari chanya zinatarajiwa kuonekana katika taasisi zote zilizoshiriki. Pamoja na masuala mengine, Herbert Maximillian Lyimo, Mtaalamu Mwandamizi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, alipata fursa ya kuelezea mwelekeo wa Serikali katika kutekeleza na kusimamia shughuli za Ufuatiliaji na Tathmini. Mafunzo haya kwa awamu ya kwanza yalihitimishwa rasmi mnamo tarehe 27 Juni, 2025 katika ofisi za EWURA mkoani Dodoma. Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Profesa Mackfallen Anasel kwa niaba ya Chuo Kikuu Mzumbe alitoa shukrani kwa Wizara ya Nishati na taasisi zake kwa ushirikiano mzuri, na kusisitiza kuwa chuo kiko tayari kuendelea kushirikiana na Wizara ya Nishati katika nyanja za ufuatiliaji na tathmini, muda wowote watakapohitajika.

None
None
None
None
None
None