News-Details

News >Details

MZUMBE MBIONI KUANZISHA KAMPASI DODOMA

MZUMBE MBIONI KUANZISHA KAMPASI DODOMA

Chuo Kikuu Mzumbe kimeonesha dhamira ya dhati ya kuanzisha Kampasi katika Mkoa wa Dodoma, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kusogeza huduma karibu na jamii na kutekeleza Mpango Mkakati wake wa maendeleo. Hatua hiyo imebainishwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. William Mwegoha, tarehe 14 Julai 2025, mara baada ya kufanya mazungumzo rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ofisini kwake jijini Dodoma. Prof. Mwegoha amesema uamuzi wa kuanzisha kampasi hiyo unatokana na umuhimu wa kuwa karibu na makao makuu ya nchi, pamoja na kuwafikia wadau mbalimbali wa elimu ya juu waliopo mkoani humo. Ameeleza kuwa Dodoma ni kitovu cha shughuli za serikali na maendeleo ya kitaifa, hivyo Mzumbe inatambua fursa na mahitaji yaliyopo kwa sasa na kwa siku zijazo. “Tunaendelea na maandalizi ya kuhakikisha kwamba Mzumbe inakuwa na uwepo wa moja kwa moja katika mkoa huu muhimu, ikiwa ni hatua ya kimkakati katika kutekeleza malengo ya Chuo na pia kuchangia juhudi za serikali katika kuimarisha elimu ya juu nchini,” alisema Prof. Mwegoha. Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amepongeza juhudi za Chuo Kikuu Mzumbe na kusisitiza kuwa mkoa wa Dodoma ni wa kimkakati na wenye kasi kubwa ya maendeleo, hivyo unahitaji uwepo wa taasisi bora za elimu kama Mzumbe. Amehimiza uanzishwaji wa programu za kisasa zitakazokidhi mahitaji ya soko la sasa na la baadaye. “Dodoma ni makao makuu ya nchi, kuna taasisi nyingi, mashirika ya umma, na sekta binafsi zinazohitaji rasilimali watu yenye weledi na ujuzi wa hali ya juu. Ni wakati muafaka sasa kwa Mzumbe kuja na programu za muda mfupi na muda mrefu ambazo zitachochea maendeleo ya mkoa huu,” alisema Mhe. Senyamule. Katika ziara hiyo ya siku moja, Prof. Mwegoha na ujumbe wake pia walikutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko. Katika mazungumzo hayo, Prof. Mwegoha alieleza kuwa Chuo kiko tayari kushirikiana na Serikali ya Jiji hilo katika kutimiza azma ya kuanzisha kampasi mpya, akisisitiza kuwa mipango ipo tayari na kinachosubiriwa kwa sasa ni utekelezaji wa hatua za awali. #tujifunzekwamaendeleoyawatu

None
None
None
None
None
None