Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China (CAU) tarehe 14 Julai 2025 kimezindua Semina ya “Teknolojia Madhubuti katika Kilimo Tanzania: Teknolojia Rahisi, Mavuno Makubwa” katika Kampasi Kuu Morogoro. Lengo kuu ni kuongeza uwezo wa maafisa ugani kutumia teknolojia shirikishi ili kuongeza tija kwa wakulima. Semina hii itafanyika kwa siku 17, kuanzia tarehe 14 hadi 30 Julai 2025, chini ya uratibu wa Mpango wa Maendeleo ya Kijamii ya Kimataifa kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (CISDET). Akifungua semina hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa A. Mussa alisema mafunzo haya ni muhimu kwa maafisa ugani ili waweze kuwafikia wakulima vijijini na kuongeza mavuno, akisisitiza kuwa yanaendana na juhudi za Serikali kuboresha kilimo kupitia mbegu bora, teknolojia za kisasa na masoko ya kidijitali. Kwa upande Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Hawa Tundui Petro, alisema semina hii ni sehemu ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kati ya Mzumbe na CAU na inadhihirisha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika maendeleo ya kilimo na tafiti. Awali Mratibu wa CISDET upande wa Mzumbe, Prof. Aurelia Kamuzora, alieleza kuwa semina inalenga kutoa suluhisho la vitendo kwa changamoto za kilimo, hasa kupitia teknolojia rahisi zinazowezekana kwa wakulima wadogo. Kwa upande wake Mshauri wa Biashara kutoka Ubalozi wa China, Bw. Chun Kun, alisisitiza fursa za kibiashara zinazotokana na ushirikiano wa Tanzania na China, huku Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo na Utafiti Wizara ya Kilimo, Bw. Godfrey Edward, akiwasihi maafisa ugani kutumia elimu hii kusaidia wakulima na kuongeza uzalishaji. Aidha,Prof. Li Xiaoyun, Profesa Mstaafu wa CAU, alieleza kuwa teknolojia hizo zinalenga kuinua maisha ya jamii vijijini kupitia Mpango wa Uhuru wa Chakula na Lishe, unaosisitiza uzalishaji wa mahindi, soya na maziwa ya soya. Vilevile Mwakilishi wa wanafunzi waliowahi kusoma CAU, Dkt. Benedicto Msangya, alieleza matarajio makubwa ya programu hii kubadilisha kilimo. Semina hii inatarajiwa kuleta mapinduzi ya kilimo kupitia uhamishaji ujuzi na uvumbuzi wa kimataifa.