Kufuatia hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Mradi wa NISHATI unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Cadiz (UCA), Hispania, kimezindua rasmi mafunzo maalumu ya “Teknolojia za Kijani kwa Pampu za Maji, Mifumo ya Kujitegemea na Mifumo Inayounganishwa na Gridi ya Taifa”, tarehe 14 Julai 2025, Kampasi Kuu Morogoro. Mafunzo haya yanalenga kuongeza ujuzi na maarifa ya watendaji wa sekta ya maji, nishati mbadala na kilimo ili kukuza uhimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Hawa Tundui Petro, aliwataka washiriki kutumia fursa hii kujenga uwezo wa kutumia teknolojia za kijani kwa vitendo, hususani katika umeme wa sola na mifumo ya umwagiliaji. Amesema mafunzo hayo yanaendana na dhamira ya Chuo Kikuu Mzumbe kuimarisha utafiti, ubunifu na ushirikiano wa kimataifa ili kutatua changamoto za mazingira na maendeleo endelevu. Kwa upande wake Amidi wa Skuli ya Utawala wa Umma na Menejimenti Chuo Kikuu Mzumbe na Mratibu wa Mradi wa NISHATI, Dkt. Idda Lyatonga Swai alifafanua kwamba mafunzo hayo yanalenga kuwa na uelewa utakaoleta suluhisho la nishati mbadala katika sekta za maji na kilimo ili kupunguza athari za tabianchi na kujenga uhimilivu wa jamii za wenyeji. Mafunzo hayo yanaendeshwa na timu ya wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Cadiz (UCA), Hispania, akiwemo mahadhri wa mifumo ya umeme na nishati mbadala, Prof. Rafael Jiménez Castañeda, Mtaalamu wa maendeleo endelevu na Uchumi, Prof. Rocío Rodríguez Barroso, na Mhandisi wa umeme katika matumizi ya programu za nishati ya jua (sola) ‘Photovoltaic (PV)’ na Teknolojia ya Maabara Gonzalo Jiménez Mañueco. Katika siku za kwanza za mafunzo haya, washiriki wamejifunza mbinu za usanifu wa miradi ya sola, pampu za maji kwa kilimo na mikakati ya kuunganisha mifumo ya ‘Photovoltaic (PV)’ na gridi za umeme, sambamba na majadiliano ya kina na mafunzo ya vitendo. Mafunzo ya NISHATI yanatarajiwa kuwa chachu ya uvumbuzi na uhimilivu, yakiwapa washiriki nyenzo muhimu za kuchangia maendeleo endelevu kwenye sekta za maji, nishati safi na kilimo hapa Afrika.