News-Details

News >Details

MZUMBE YAKABIDHI VITABU KWA TAASISI MBILI DODOMA

MZUMBE YAKABIDHI VITABU KWA TAASISI MBILI DODOMA

Chuo Kikuu Mzumbe kimekabidhi rasmi mchango wa jumla ya vitabu 1264 kwa taasisi mbili jijini Dodoma mnamo tarehe 29 Julai 2025 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na kuongeza upatikanaji wa maarifa kwa watumishi na wadau wa elimu. Ujumbe wa Chuo Kikuu Mzumbe ukiongozwa na Maafisa wa Maktaba, uliwasilisha vitabu hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Huduma za Maktaba. Katika ziara ya kukabidhi vitabu vilivyofanyika katika ofisi za Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, ujumbe huo ulipokelewa na Katibu Mtendaji wa Tume, Bw. George Mandepo, pamoja na viongozi waandamizi wa Tume hiyo. Vitabu 448 vilikabidhiwa rasmi kwa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, ambapo Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Bw. George Mandepo, alipokea pia nakala za Mzumbe Journal kutoka kwa Bi. Yulita Michael, Mkutubi wa Chuo Kikuu Mzumbe. Hatua hii inalenga kuchangia katika kukuza maarifa ya kisheria kwa watumishi wa umma na wadau wa sekta ya sheria nchini. Aidha, vitabu vingine 816 vilikabidhiwa kwa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, ambapo pande zote mbili zilieleza dhamira ya kuendeleza ushirikiano wa karibu kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu na utafiti katika maeneo yao ya kazi. Tukio hili limeweka msingi mzuri wa ushirikiano wa kimaarifa kati ya taasisi hizo, ambapo imekubaliwa kuwa ushirikiano huo utaendelezwa kupitia njia mbalimbali za kitaaluma, zikiwemo warsha, tafiti za pamoja na mabadilishano ya nyenzo za kielimu.

None
None
None