Chuo Kikuu Mzumbe kimeungana na taasisi mbalimbali kushiriki katika Maonesho ya 32 ya Nanenane Kanda ya Mashariki, yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu J. K. Nyerere, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti 2025. Maonesho haya ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo: “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025.” Akizungumza Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko, Bi. Lulu Mussa ameeleza kuwa kupitia ushiriki wake, Chuo Kikuu Mzumbe kinajidhihirisha kama taasisi mahiri ya elimu ya juu inayowekeza katika ujenzi wa jamii yenye uelewa, ubunifu na uwezo wa kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii. Aidha, ameeleza kuwa chuo kinatoa huduma mbalimbali zikiwemo: Elimu kuhusu uchaguzi wa kozi na vigezo vya kujiunga na chuo kwa wanafunzi watarajiwa, Ushauri wa kitaaluma kwa vijana wanaotafuta mwelekeo sahihi wa masomo yao ya juu, Huduma ya udahili wa papo kwa papo kwa waombaji wa programu za Astashahada, Stashahada na Shahada kwa mwaka wa masomo 2025/2026, Usajili wa wanachuo waliomaliza masomo (Alumni) wa zamani wa IDM/Mzumbe kwenye kanzidata maalumu, Huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi kupitia Kituo cha Msaada wa Kisheria cha chuo, Maonesho ya bunifu mbalimbali na huduma za kijasiriamali zinazotekelezwa na vitengo vya chuo na Utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kitaaluma na kimazingira, ikiwemo Mradi wa HEET (Higher Education for Economic Transformation). Ushiriki wa Chuo Kikuu Mzumbe katika maonesho haya unalenga kuonesha mchango wake katika kuendeleza sekta ya kilimo na maendeleo ya kijamii kupitia elimu, tafiti, ubunifu na ushirikiano wa karibu na jamii. Wananchi wote wanakaribishwa kutembelea banda la Mzumbe ili kunufaika na huduma zinazotolewa.