Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima katika Uongozi ya Chuo Kikuu Mzumbe ambapo katika hotuba yake amesema kuwa kiongozi ni mtumishi anayeendeleza ya jana, anayebuni, kuibua na kutekeleza ya leo na akaacha ya kuendelezwa kwa ajili ya kesho. Rais Dkt. Samia ametunukiwa shahada hiyo leo Novemba 24, 2024 na Mkuu wa Chuo hicho, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein kwenye mahafali ya 23 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika eneo la Maekani, Kampasi Kuu Morogoro. Rais Dkt. Samia amesema kuwa maeneo yote aliyopita yamemjenga na kumfungulia upeo wa maarifa na kuweza kufanya mambo mengi ambayo yanaendelea kutekelezwa sasa. "Mapito ya safari yangu katika nyadhifa mbalimbali yamenipa maarifa ya kuweza kuwaongoza wenzangu katika kulitumikia Taifa hili. Mtindo wangu wa uongozi umejengeka juu ya misingi mikuu mitatu ikiwemo; ushirikishwaji, maamuzi yanayozingatia ushahidi na kutanguliza maslahi ya taifa." Amesema Rais Dkt. Samia. Katika msingi wa ushirikishwaji, Rais Samia amesisitiza kuwa nchi ni ya Watanzania wote na kila mmoja ana haki ya kuchangia katika ujenzi wa taifa hilo ambapo alipokabidhiwa dhamana ya kuwa Rais, aliona haja ya kuwaunganisha Watanzania ili kurudisha hisia ya utaifa na wote kuishi kama watu wa Taifa moja. Vile vile, alianzisha falsafa ya R4 kwani aliamini kuwa kuzungumza, kupata muafaka wa namna ya kuendesha mambo na kustahimiliana kutaleta utulivu mkubwa utakaowezesha kufanya kazi na kuwahudumia wananchi kwa usalama na amani na kuwa na maendeleo nchini. Amesema, msingi wa uamuzi unaozingatia ushahidi, ni msingi unaoiongoza nchi katika kufanya mageuzi na kuendesha shughuli mbalimbali za serikali ikiwemo ushahidi unaohusu masuala ya ufuatiliaji na tathimini ambapo zimeundwa Kamati, Vikosi Kazi na Tume kadhaa kwa ajili ya kufanya utafiti jinsi ya kuendesha shughuli mbalimbali za serikali.