Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert John Chalamila, ametembelea banda la Chuo Kikuu Mzumbe tarehe 6 Agosti 2025 katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea kufanyika kwenye viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere - Nanenane, Morogoro. Ametoa pongezi kwa chuo hicho kwa kusimamia ubora wa elimu na kuhimiza utoaji wa ujuzi wa vitendo kwa wanafunzi uendelee kuimarishwa zaidi. Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Mhe. Chalamila alisisitiza kuwa maendeleo ya taifa yanahitaji elimu inayomwandaa mwanafunzi kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi badala ya kuishia kwenye nadharia pekee. "Hatutaki kuona vijana wakiwa na vyeti tu bila ujuzi. Tunahitaji elimu yenye matokeo, inayojenga maarifa, ubunifu na ushindani," alisisitiza Mhe. Chalamila. Aidha, alitambua mchango wa Mzumbe kama taasisi inayotoa elimu bora na kuandaa wataalamu wanaoendelea kuwa msaada mkubwa kwa taifa. Mhe. Chalamila pia alitoa rai kwa uongozi wa chuo kuendelea kujikita katika kutoa elimu inayozingatia mahitaji ya soko la ajira ili mud ana rasilimali zinazowekezwa katika elimu isiwe kazi bure. Kwa upande wake Afisa Masoko wa Chuo Kikuu Mzumbe, Bi. Gloria Mushi, alieleza kuwa Chuo kinatoa kozi mbalimbali kuanzia ngazi ya stashahada hadi shahada ya uzamivu, pamoja na huduma za ushauri wa kitaalamu kwa jamii. Alibainisha kuwa Mzumbe imejipanga kutoa wahitimu wenye ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa, sambamba na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa. Maonesho ya Nanenane 2025 yenye kaulimbiu: “Chagua Viongozi Bora kwa maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”, yamekuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za elimu kama Mzumbe kuonesha mchango wao katika maendeleo ya sekta elimu kupitia shughuli za Kitaaluma, Utafiti, Ushauri wa Kitaalamu na kuifikia jamii kwa namna tofautitofauti.