Chuo Kikuu Mzumbe kimepitia na kuthibitisha maudhui ya Somo la Elimu ya Katiba na Maadili (Constitution and Ethics) ambalo litaanza kufundishwa chuoni kwa lengo la kujenga ufahamu na uelewa wa Katiba, pamoja na kulinda na kuthamini rasilimali za taifa. Hatua hii imefikiwa kupitia kikao cha pamoja kati ya Menejimenti na wataalamu wa Chuo Kikuu Mzumbe wakishirikiana na Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria, kilichofanyika leo, mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Wizara hiyo jijini Dodoma. Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha, aliambatana na ujumbe wake kushiriki katika kikao hicho, ambacho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Eliakim Maswi na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Katiba na Sheria. Somo hili litakapozinduliwa rasmi, litafundishwa katika ngazi zote kuanzia Astashahada, Stashahada, Shahada hadi Shahada ya Umahiri, huku pia kukiwa na mpango wa kulifikisha kwa wananchi walio nje ya mfumo rasmi wa elimu kupitia kozi za muda mfupi. Vilevile, kikao hicho kilijadili maandalizi ya Kongamano litakalowakutanisha wadau mbalimbali wa elimu, ikiwa ni pamoja na taasisi za elimu ya juu zitakazoshiriki katika utoaji wa elimu hii, kwa lengo la kuimarisha uzalendo na mshikamano wa kitaifa. Kwa kuanzisha somo hili, Chuo Kikuu Mzumbe kinachukua hatua madhubuti katika kulea kizazi kinachotambua wajibu wake wa kikatiba, kinachoenzi maadili, na chenye dira ya kulinda maslahi ya Taifa kwa maendeleo endelevu.