Chuo Kikuu Mzumbe kimeendesha mafunzo ya siku mbili kwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi na wahadhiri wake katika kutumia Miundo Mikubwa ya Lugha (LLMs) kutengeneza Mifumo Mahiri ya Kufundisha yenye kuzingatia muktadha (Contextualized Intelligent Tutoring Systems). Mafunzo haya yamefanyika kuanzia tarehe 7 hadi 8 Agosti 2025, katika Ukumbi wa Morogoro Hotel, mkoani Morogoro. Mafunzo haya, yaliyoandaliwa kupitia miradi ya AI4STEM, Data2Info, na FoundationAI, yamehusisha wanafunzi wa Shahada ya Awali na Shahada ya Umahiri katika fani ya TEHAMA pamoja na wahadhiri kutoka Idara ya Masomo ya Sayansi ya Kompyuta. Yamefunguliwa rasmi na Dkt. Joseph Sungau, Mtiva wa Kitivo cha Sayansi na Teknolojia, ambaye alisisitiza umuhimu wa kuunganisha Akili Mnemba katika shughuli za elimu na taaluma za kila siku. “Hatuwezi kuepuka Akili Mnemba. Tupo katika zama ambapo matumizi ya intaneti ni nyenzo muhimu ya kufanya maamuzi sahihi katika kila sekta. Uundaji wa mifumo mahiri ya kufundisha ni nguzo muhimu ya mradi wa AI4STEM unaolenga shule za msingi nchini Tanzania,” alisisitiza Dkt. Sungau. Kupitia mafunzo haya, washiriki wamejifunza mbinu za awali za kubuni mifumo mahiri inayotumia Akili Mnemba ili kuboresha ujifunzaji na ufundishaji wa kidijitali, huku wakizingatia mazingira halisi ya Kiafrika. Mafunzo haya yameendeshwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Ghent, Bi. Eva Verhelst na Bw. Ruben Janssens, waliotoa mwongozo wa kitaalamu kuhusu namna ya kubuni na kusimamia mifumo hiyo. Kufikia mwisho wa mafunzo haya, washiriki wanatarajiwa kuwa na uwezo wa kutunga, kubuni na kutumia mifumo mahiri ya kufundisha inayokidhi mahitaji ya ndani, hatua muhimu kuelekea mageuzi ya elimu yanayochochewa na Akili Mnemba nchini.