Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya kimehitimisha rasmi ushiriki wa maonesho ya Nanenane ya mwaka 2025 yaliyofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, kwa mafanikio makubwa na mwitikio chanya kutoka kwa wananchi tarehe 8 Agosti 2025. Katika kipindi chote cha maonesho, banda la chuo lilipokea wageni kutoka makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa shule za sekondari, wazazi, wadau wa elimu, pamoja na wahitimu wa Chuo hicho. Wageni walipata nafasi ya kufahamu kwa kina programu mbalimbali zinazotolewa Chuoni hapo, huduma ya udahili, bunifu za kibiashara kutoka kwa wanafunzi, msaada wa kisheria na usajili wa wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe. Akizungumza katika siku ya kuhitimisha maonesho hayo, Afisa Uhusiano wa Ndaki ya Mbeya, Bi. Cecilia Assenga alieleza kuwa maonesho hayo yametoa jukwaa muhimu kwa taasisi kujitangaza, kuhamasisha udahili, na kujenga mahusiano mapya na wadau wa elimu. “Tunajivunia mwitikio mkubwa wa wananchi waliotembelea banda letu. Tumewafikia vijana wengi waliovutiwa na ubora wa programu zinazotolewa na Chuo Kikuu Mzumbe na tumeongeza uelewa kwa jamii kuhusu nafasi ya elimu ya juu katika maendeleo ya taifa,” alieleza Bi. Assenga. Kupitia maonesho hayo, Ndaki ya Mbeya imefanikiwa kufikia taasisi mbalimbali za Umma na binafsi katika kujenga mahusiano bora na mashirikiano ya kimkakati ili kuongeza ufanisi kwenye sekta ya elimu na maendeleo ya wanafunzi na taifa kwa ujumla. Vilevile, Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya kilipokea cheti cha ushiriki wa maonesho hayo. Ushiriki wa Ndaki ya Mbeya katika maonesho hayo pia umeonesha uwezo wa taasisi katika kuwasilisha elimu, maarifa na utafiti kwa jamii, sambamba na kuonesha mchango wake katika kuendeleza sekta ya elimu nchini. Ndaki ya Mbeya itaendelea kushiriki katika matukio mbalimbali ya kijamii ili kuendeleza dhamira yake ya kutoa elimu bora, jumuishi na inayolenga maendeleo endelevu kwa watu.