Chuo Kikuu Mzumbe kimeendesha Warsha ya Mafunzo kwa Wanafunzi wa Shahada ya Uzamivu kuhusu “Uandishi wa Makala za Kitaaluma kwa Njia ya Kufanya Mapitio ya Maandiko kwa Uchanganuzi Thabiti wa Kiuhakiki”, iliyofanyika katika Ukumbi wa Fanon, Kampasi Kuu Morogoro mnamo tarehe 13 Agosti 2025. Akifungua rasmi warsha hiyo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui Petro, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha washiriki kutambua kanuni na mbinu za uhakiki wa kitaratibu na uchambuzi shirikishi wa takwimu, pamoja na kuwapa mwongozo wa hatua za upangaji na uandishi wa makala za kisayansi. Prof. Tundui alibainisha kuwa mafunzo hayo pia yanalenga kuwafundisha washiriki matumizi ya zana za programu kwa usimamizi wa marejeo na uchambuzi shirikishi wa takwimu, kuongeza uelewa na namna bora ya kuchagua jarida sahihi, kuelewa matarajio ya uhakiki wa kitaalamu wa maandiko, na kuzingatia maadili ya uchapishaji wa kitaaluma. Akiwasilisha mada kuu, Mwezeshaji kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Joseph Magali, alizungumzia Uhakiki wa Fasihi na mbinu za kupata taarifa muhimu kutoka makala za kitaaluma. Alisisitiza umuhimu wa uchambuzi wa kina wa maandiko ili kupata msingi imara wa tafiti mpya. Aidha, Washiriki wa warsha walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata majibu ya kina kutoka kwa wawezeshaji, jambo lililoongeza uelewa wao wa mbinu za utafiti na uandishi wa kitaaluma. Washiriki pia walishiriki michezo mbalimbali ikiwemo riadha, mpira wa miguu, karata, kutembea na magunia, na mbio za mayai, ili kujenga mshikamano, kushirikiana, na kupumzisha akili baada ya mafunzo ya kitaaluma. Warsha hii imeonyesha dhamira ya Chuo Kikuu Mzumbe katika kuendeleza ubora wa utafiti na machapisho ya kitaaluma, sambamba na kukuza ustawi wa kijamii wa wanafunzi wake.