Chuo Kikuu Mzumbe, kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET Project), kwa kushirikiana na East Spark Project pamoja na Kurugenzi ya Utafiti, Machapisho na Masomo ya Uzamili (DRPS), kimeandaa mafunzo ya siku mbili kwa wanataaluma wa chuo hicho kuhusu usimamizi bora wa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili. Mafunzo hayo yameanza leo, tarehe 19 Agosti 2025, katika Hoteli ya Morena, mkoani Morogoro, yakihusisha washiriki wanataaluma kutoka vitivo na ndaki zote za Chuo Kikuu Mzumbe. Akiwakaribisha washiriki kwa niaba ya Mkurugenzi wa Utafiti, Machapisho na Masomo ya Uzamili, Dkt. Juma Buhimila, Mkuu wa Idara ya Masomo ya Uzamili, aliwahimiza washiriki kufuatilia mafunzo hayo kwa makini huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na wasimamizi wenye uelewa wa kina na weledi katika mchakato mzima wa Shahada ya Uzamili. Miongoni mwa wakufunzi wa mafunzo haya ni Profesa Fanuel Lampiao kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya cha Kamuzu – Malawi, ambaye aliwasilisha mada kuhusu "Kuimarisha ujuzi wa uandishi na uwezo wa kuchapisha kazi za kitaaluma." Prof. Lampiao aliwataja walimu kuwa Shahada ya Uzamili si tu chombo cha kujijengea taaluma, bali ni njia muhimu ya kuzalisha maarifa mapya yanayochangia maendeleo ya taifa na bara la Afrika kwa ujumla. Mafunzo haya yametilia mkazo umuhimu wa kuimarisha uwezo wa wasimamizi katika usimamizi wa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili, kupitia mada mbalimbali zilizofundishwa na wawezeshaji. Washiriki walipata uelewa wa kina juu ya hatua muhimu za kuchagua, kuwasajili, na kuongoza wanafunzi wa Shahada ya Uzamili kufanikisha utafiti wao kikamilifu. #tujifunzekwamaendeleoyawatu