Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (United Nations Development Programme – UNDP) wametia saini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) katika hafla iliyofanyika tarehe 2 Septemba 2025 Chuo kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro, hatua inayofungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kitaaluma na kimaendeleo kwa mustakabali wa elimu ya juu nchini Tanzania. Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Allen Mushi alieleza kuwa makubaliano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa uwekezaji utakaosaidia chuo kujiimarisha kifedha kwa njia mbadala. Alibainisha kuwa sambamba na hilo, chuo kitajenga jengo jipya ambalo litakuwa ni kitega uchumi katika Ndaki ya Dar es Salaam, eneo la Upanga, litakalotumika pia kwa shughuli za kitaaluma "Dokezo la mradi huo litawavutia wawekezaji wengi kwani litaandikwa na wataalamu katika timu inayoundwa ambayo inahusisha Wataalamu wa ndani ya chuo pamoja na washirika kutoka wizara na taasisi mbalimbali ikiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MoEST), Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Center)". Aliongeza Prof. Mushi Aidha, alisisitiza kuwa miradi hiyo itazingatia Hati za Kijani (Green Bonds) zinazolenga ujenzi rafiki wa mazingira na kuendesha shughuli kwa kuzingatia misingi ya Utawala wa Mazingira, Jamii na Usimamizi Bora (Environmental, Social and Governance – ESG). Awali, Mkurugenzi wa Mipango wa Chuo Kikuu Mzumbe, Bw. Edwin Ninde, alisema makubaliano hayo ni ishara ya ndoto za muda mrefu za chuo kuanza kutimia na yanatoa fursa ya kuimarisha nafasi ya Mzumbe kama kitovu cha ujuzi na ubunifu nchini. Alisisitiza kuwa kupitia ushirikiano huo, chuo kitapanua upeo wake wa kielimu na kijamii sambamba na kujiimarisha katika nyanja za kiuchumi. Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara, alisema makubaliano hayo yanalenga kuimarisha ubadilishanaji wa maarifa, kukuza vipaji vya wanafunzi na wafanyakazi, na kuendeleza shughuli za kiuchumi za chuo ili kuchangia katika azma ya taifa kufikia uchumi wa kipato cha kati. “Hii ni hati ya makubaliano ya kwanza kabisa kati ya UNDP na taasisi ya elimu ya juu nchini Tanzania na tunatarajia ushirikiano zaidi na vyuo vingine. Tuko tayari kushirikiana na skuli, vitivo na wanafunzi wote wa Mzumbe ili kuonesha uwezo mkubwa wa chuo hiki kwa maendeleo ya baadaye,” alisema Bw. Komatsubara. Makubaliano haya yanatarajiwa kufungua milango ya fursa mpya za kielimu, kuimarisha ubora wa tafiti, kupanua kampasi, na kuhamasisha rasilimali endelevu. Hii ni hatua inayoweka Chuo Kikuu Mzumbe katika nafasi ya kipekee ya kuchangia si tu maendeleo ya taifa, bali pia kulisaidia bara la Afrika kwa mfano wa ushirikiano wa kimkakati unaojali elimu, ubunifu na utunzaji wa mazingira.