News-Details

News >Details

DKT. SHEIN APOKEA TAARIFA YA CHUO, ARIDHISHWA NA KASI YA MAENDELEO

DKT. SHEIN APOKEA TAARIFA YA CHUO, ARIDHISHWA NA KASI YA MAENDELEO

Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, tarehe 4 Septemba 2025 jijini Dar es Salaam, amepokea taarifa ya maendeleo ya Chuo Kikuu Mzumbe na kueleza kuridhishwa na hatua kubwa zilizopatikana ndani ya mwaka mmoja tangu taarifa ya mwisho Novemba 2024. Dkt. Shein alipongeza Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Prof. Saida Yahya-Othman, kwa uongozi thabiti na usimamizi mzuri wa mipango ya maendeleo ya Chuo, sambamba na Menejimenti na wafanyakazi kwa kujituma chini ya uongozi wa Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha. Akiweka msisitizo, Dkt. Shein alipongeza ushirikiano wa Chuo na taasisi mbalimbali, hususan mpango wa kuandaa mtaala wa Elimu ya Katiba, Uraia na Uzalendo kwa vyuo vikuu, ambapo Mzumbe imekuwa mwanzilishi. Alisisitiza umuhimu wa mafunzo ya maadili na uzalendo ili kuwajenga wanafunzi na vijana kutambua wajibu wao wa kulinda rasilimali na tunu za taifa. “Nimefurahishwa sana na taarifa hii, hasa mpango wa kuimarisha uzalendo na maadili kwa vijana wetu,” alisema Dkt. Shein. Kwa upande wake, Prof. Saida Yahya-Othman alimshukuru Mkuu wa Chuo kwa mwongozo wake unaoendelea kuhamasisha utekelezaji wa mipango, jambo lililowezesha Mzumbe kuongeza kozi mpya, mapato ya ndani na kasi ya maendeleo. Awali, Prof. Mwegoha alieleza kuwa Chuo kimeongeza idadi ya wanafunzi kwa asilimia 9.12, kuajiri na kuwaendeleza kitaaluma wafanyakazi, na kusaini mikataba ya ushirikiano 30 huku mingine 45 ikikamilishwa. Pia alibainisha ushirikiano mpya na UNDP kwa uwekezaji, ikiwemo mpango wa kituo cha uwekezaji katika Kampasi ya Dar es Salaam. Aidha, maboresho ya miundombinu yameendelea katika Kampasi za Morogoro, Dar es Salaam na Mbeya pamoja na ujenzi wa Kampasi mpya Jijini Tanga na hatua iliyofikiwa ya mradi wa hosteli za wanafunzi wa kike katika kampasi ya Mbeya Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Makamu Mkuu wa chuo Kikuu Mzumbe - Mipango, Fedha na Utawala, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma, Utafiti na Ushauri, Kaimu Katibu wa Baraza, Msaidizi Mahsusi wa Makamu Mkuu wa Chuo na Maafisa wa kitengo cha Mawasiliano na masoko wa Chuo kikuu Mzumbe.

None
None
None
None
None
None
None