News-Details

News >Details

DC MKINGA AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA KAMPASI MPYA YA MZUMBE TANGA

DC MKINGA AKAGUA MAENDELEO YA  UJENZI WA KAMPASI MPYA YA MZUMBE TANGA

Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe. Gilbert Kalima, amepongeza kasi ya ujenzi wa kampasi mpya ya Chuo Kikuu Mzumbe inayojengwa katika wilaya ya Mkinga mkoani Tanga akisema ni hatua ya kihistoria kwa maendeleo ya elimu ya juu katika mkoa huo na kueleza kuridhishwa kwake na hatua za ujenzi ambapo aliipongeza Menejiment ya chuo kwa usimamizi mzuri unaopelekea Mkandarasi kufanya kazi kwa juhudi na kasi kubwa. Ameyasema hayo Septemba 4, 2025, alipotembelea eneo la mradi akiwa ameongozana na Kamati Tendaji ya Wilaya ambapo walikagua maendeleo na kujadiliana namna wilaya itakavyoshiriki katika kufanikisha kukamilika kwa ujenzi huo. "Tulikuwa na hamu kubwa ya kuwa na taasisi ya elimu ya juu wilayani kwetu. Hii ni historia kubwa na chachu ya maendeleo kwa Wilaya ya Mkinga. Nawashukuru sana Chuo Kikuu Mzumbe kwa uamuzi huu,” alisema Mkuu wa wilaya Aidha, Mhe. Kalima aliahidi kushirikiana kwa karibu na viongozi na wadau husika katika kuhakikisha changamoto zilizopo zinashughulikiwa ili mradi huo mkubwa wa kimkakati ukamilike kwa wakati. Awali akimpokea Mkuu wa Wilayq,Kaimu Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Mohamed Ghasia alieleza dhamira ya chuo kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kampasi hiyo inakamilika kwa wakati, ikiwemo maandalizi ya upatikanaji wa huduma za afya na mikakati ya kuongeza idadi ya wanafunzi watakaojiunga katika kampasi hiyo mpya. Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa HEET upande wa ujenzi, QS. Prosper Leonard, alisemq kasi ya ujenzi inaendelea kwa mafanikio makubwa ambapo sehemu ya kwanza ya ujenzi (Lot I) imefikia asilimia 67 ya utekelezaji na kufafanua kuwa sehemu hiyo inahusisha majengo makuu matatu ambayo ni Jengo la Masomo, Kituo cha Afya na Cafeteria na kuongeza kuwa 'Lot II' nayo imepiga hatua kubwa kwa kufikia asilimia 68 ya maendeleo, ikijumuisha majengo mawili ya hosteli za wanafunzi, nyumba nne za watumishi pamoja na mfumo wa maji safi na maji taka. Ujenzi wa kampasi hiyo mpya unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo siyo tu kwa Wilaya ya Mkinga bali pia kwa mkoa mzima wa Tanga, kwa kuongeza fursa za elimu ya juu, kukuza ajira na kuchochea uchumi wa eneo hilo.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None