News-Details

News >Details

WAZIRI MKUU AWAPONGEZA MZUMBE KWA KUDHAMINI KONGAMANO LA NNE LA UFUATILIAJI, TATHMINI NA UJIFUNZAJI

WAZIRI MKUU AWAPONGEZA MZUMBE KWA KUDHAMINI KONGAMANO LA NNE LA UFUATILIAJI, TATHMINI NA UJIFUNZAJI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amewapongeza wadhamini wa Kongamano la Kimataifa la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (Monitoring, Evaluation and Learning – MEL), wakiwemo Chuo Kikuu Mzumbe, kwa kudhamini kongamano hilo linaloendelea katika Hoteli ya Malaika Beach Resort, Jijini Mwanza. Kongamano hilo linawakutanisha wadau wa ndani na nje ya Tanzania kutoka sekta na taasisi mbalimbali. Akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu alisema kongamano la mwaka huu limekuwa na mafanikio makubwa na kuonesha mchango wa sekta ya ufuatiliaji na tathmini katika maendeleo ya taifa. Alibainisha kuwa sekta hiyo ni nyenzo muhimu ya kufuatilia utekelezaji wa dira ya maendeleo ya taifa na usimamizi wa miradi mikubwa ya huduma za kijamii. Aliwashukuru wadhamini na washiriki kwa mchango wao katika kufanikisha kongamano hilo. Aidha, Waziri Mkuu aliagiza kuanzishwa kwa mchakato wa kuandaa Sheria ya Tathmini na Ufuatiliaji na kuzitaka taasisi kuanzisha vitengo husika. Pia aliagiza taasisi zenye vitengo hivyo ziendelee kujenga uwezo wa wataalamu wa sekta hiyo ili kuimarisha mifumo ya kitaifa. Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, alieleza udhamini wa chuo hicho ni sehemu ya kutambua nafasi ya sekta ya tathmini na ufuatiliaji katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050. Hivyo kama taasisi inayozalisha wataalamu wa sekta hiyo, Mzumbe imeona wajibu wa kutoa mchango wa kitaaluma, kitaalamu na kifedha. “Ufadhili huu ni sehemu ya mkakati wa Chuo chetu kuhakikisha kinakuwa chachu ya mabadiliko na kusaidia kusukuma ajenda ya Serikali ya kuimarisha mifumo ya usimamizi wa utendaji kwa maendeleo ya Taifa.” alisema Prof. Mwegoha. Kongamano hili lenye kaulimbiu: Kuimarisha ufuatiliaji na tathmini katika ngazi ya jamii ili kuleta maendeleo endelevu, limekutanisha zaidi ya washiriki 1,000 kutoka nchi 18, wakiwemo viongozi wa serikali, mabalozi, sekta binafsi, taasisi za elimu, wanafunzi na wadau wa maendeleo.

None
None
None
None
None
None
None
None
None