Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha ameeleza nafasi ya Vyuo katika kuimarisha taaluma ya Ufuatiliaji, Tathmini na Ujifunzaji (Monitoring, Evaluation and Learning – MEL) ili kufanikisha malengo ya DIRA 2050. Akiwasilisha mada elekezi (keynote address) kwa wadau walioshiriki Kongamano la Nne la MEL, siku ya tatu tarehe 12 Septemba 2025 katika Hoteli ya Malaika Beach Resort, Jijini Mwanza. Prof. Mwegoha alieleza kuwa vyuo vikuu vina wajibu mkubwa wa kujenga uwezo wa kitaaluma na kiutafiti kwa kuzalisha wataalamu wanaoendana na mabadiliko na kasi ya maendeleo, kufanya tafiti bunifu na kutoa maarifa yanayolenga muktadha wa Kiafrika ili kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi huku akitolea mfano Chuo Kikuu Mzumbe ambacho tayari kinatoa taaluma ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza kwa ngazi ya Shahada ya Awali pamoja na Shahada ya Umahiri. Aidha, Prof. Mwegoha alisisitiza kuwa utekelezaji wa DIRA 2050 unahitaji mifumo thabiti ya ufuatiliaji na tathmini inayomilikiwa na jamii badala ya kutegemea wafadhili pekee. “DIRA 2050 ni ahadi ya kizazi. Ili iwe halisi, tathmini lazima iwe ya ndani, shirikishi na izingatie mahitaji ya wananchi. Hii ni safari ya mshikamano na uthabiti,” alisema Prof. Mwegoha. Prof. Mwegoha alibainisha maeneo manne muhimu ya mapinduzi ya MEL chini ya DIRA 2050 kuwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia na data, kupunguza utegemezi wa mifumo ya kigeni, kuunganisha taaluma mbalimbali, na kujenga daraja kati ya sera na utekelezaji. Kongamano lenye kaulimbiu “Kuimarisha ufuatiliaji na tathmini katika ngazi ya jamii ili kuleta maendeleo endelevu” limekutanisha zaidi ya washiriki 1,000 kutoka nchi 18, wakiwemo viongozi wa serikali, mabalozi, sekta binafsi, taasisi za elimu, wanafunzi na wadau wa maendeleo.