News-Details

News >Details

MZUMBE YANG’ARA KATIKA KONGAMANO LA NNE LA MEL 2025

MZUMBE YANG’ARA KATIKA KONGAMANO LA NNE LA MEL 2025

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (Mb.) amewapongeza wadau walioshiriki Kongamano la Nne la Ufuatiliaji, Tathmini na Ujifunzaji (Monitoring, Evaluation and Learning – MEL) 2025, huku akizitaka taasisi kuendelea kushirikiana katika kuandaa na kufanikisha makongamano yajayo kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa. Akizungumza Septemba 12, 2025 wakati wa kufunga rasmi kongamano hilo, Dkt. Biteko alisema kuwa ufuatiliaji na tathmini ni nyenzo muhimu katika kufanikisha malengo ya DIRA 2050 huku akiwataka wataalamu wa tathmini na ufuatiliaji kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa haki na mujibu wa sheria bila kuogopa kuchukiwa ama kubezwa, na akatoa wito kwa viongozi wa taasisi za Serikali kuwapeleka watendaji wao kujifunza zaidi kupitia makongamano na mijadala ya kitaaluma ili kuongeza ufanisi wa utendaji wa taasisi na taifa kwa ujumla. Katika kilele cha hafla hiyo, Dkt. Biteko alikabidhi tuzo za ushiriki na udhamini kwa taasisi zilizochangia kufanikisha kongamano hilo. Kwa upande wa Chuo Kikuu Mzumbe, tuzo hiyo ilipokelewa na Mhadhiri wa Uchumi na Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET, Dkt. Lihoya Chamwali, kwa niaba ya chuo. Chuo Kikuu Mzumbe kimeshiriki kikamilifu kongamano hilo kama mmoja wa wadhamini wakuu na mdau muhimu katika taaluma ya Ufuatiliaji, Tathmini na Ujifunzaji, ambayo hufundishwa chuoni kwa ngazi ya Shahada ya Awali na Shahada ya Umahiri. Kongamano hili, lililobeba kaulimbiu: Ufuatiliaji na Tathmini inayoongozwa na jamii: Kujenga uwezo wa ndani na umiliki wa Ufuatiliaji, Tathmini Na Ujifunzaji kwa athari endelevu yaani “Community-Led M&E: Building Local Capacity and MEL Ownership for Sustainable Impact”, limefanyika kuanzia Septemba 10 – 13, 2025 katika Hoteli ya Malaika Beach Resort, Jijini Mwanza. Zaidi ya washiriki 1,000 kutoka nchi 18 walihudhuria, wakiwemo viongozi wa Serikali, mabalozi, taasisi za elimu, sekta binafsi, vijana na wadau wa maendeleo. Kupitia ushiriki wake, Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kuthibitisha nafasi yake kama kinara wa kitaaluma na kiutafiti, kinachochangia moja kwa moja katika utekelezaji wa agenda za kitaifa na kimataifa za maendeleo endelevu.

None
None
None
None
None
None
None