Chuo Kikuu Mzumbe kimeendesha kikao maalumu kwa wanataaluma, kilichoongozwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui Petro, leo tarehe 11 Septemba 2025, Kampasi Kuu Morogoro, kwa lengo la kuweka mikakati ya utekelezaji wa majukumu ya kitaaluma katika mwaka mpya wa masomo. Kikao hicho kilihusisha wanataaluma kutoka vitivo mbalimbali na skuli za chuo, ambapo mjadala mkuu ulijikita katika utekelezaji wa programu mpya za Uzamili zilizopitishwa hivi karibuni, ambazo zitafundishwa kwa mfumo wa ujifunzaji mseto (blended learning mode). Washiriki walipata pia fursa ya kujifunza mbinu za kuandaa maudhui yanayofaa kwa mfumo huu, kuhakikisha elimu inawafikia wanafunzi kwa ufanisi na inachangia maarifa ya vitendo. Akitoa maelezo zaidi, Prof. Hawa Tundui alisisitiza wajibu wa wanataaluma katika kujenga mazingira bora ya ujifunzaji kwa wanafunzi, akibainisha kuwa kila mwalimu anapaswa kuboresha mbinu zake za ufundishaji ili kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa stahiki kulingana na ngazi zao za masomo. Aliongeza kuwa ni muhimu kuweka utofauti kati ya kile kinachofundishwa kwa wanafunzi wa ngazi ya Cheti na wale wa Shahada, ili kila kundi lipate stadi na ujuzi unaohitajika kwa maendeleo yao ya kitaaluma na maisha ya kazi badaa ya kuhitimu masomo yao. Prof. Hawa Tundui pia alisisitiza umuhimu wa walimu kuandaa maswali na tathmini zinazochochea fikra za kina (critical thinking) kwa wanafunzi, ili kuwajengea uwezo wa kutafuta majibu na ubunifu wa suluhisho kwa changamoto wanazokutana nazo. “Kila mwanafunzi anapaswa kujifunza kutafuta majibu na kufikiri kwa mapana, si kukariri tu,” alisema. Aidha, aliongeza kuwa walimu wanalo jukumu la kuwatambua wanafunzi wenye mahitaji maalum ya ujifunzaji na kuwasaidia kulingana na uwezo wao, ili kila mmoja aweze kunufaika na elimu anayopata. Alisisitiza pia kuwa mtihani na tathmini ni sehemu muhimu ya kupima kama mwanafunzi amejifunza kwa ufanisi, hivyo maandalizi na ufuatiliaji wake vinapaswa kutiliwa mkazo. Kwa mujibu wa Prof. Hawa Tundui, utekelezaji wa mikakati hii utaifanya Mzumbe kuendelea kuwa kitovu cha maarifa na ubunifu, chenye mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kupitia elimu bora na yenye kuendana na mahitaji ya jamii.