Bi. Mwanahamisi Salehe, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka Idara ya Uchumi, Kitivo cha Sayansi za Jamii (FSS), Chuo Kikuu Mzumbe, amefanikisha hatua kubwa katika safari yake ya kitaaluma baada ya kutetea tasnifu yake kwa mafanikio makubwa. Utetezi huo umefanyika tarehe 12 Septemba 2025, katika Kampasi Morogoro, mbele ya jopo la watahini lililoongozwa na Prof. Ernest Kihanga, huku Prof. Jennifer Sesabo akiwa msimamizi mkuu wa utafiti. Utafiti wake ulijikita kwenye “Ujasiriamali endelevu na utendaji wa biashara ndogo na za kati za uvuvi nchini Tanzania”, ambapo alionyesha jinsi ujasiriamali endelevu unavyoweza kuchochea maendeleo na kuongeza tija ya biashara ndogo na za kati katika sekta ya uvuvi. Akizungumza katika utetezi wake, Bi. Salehe alisisitiza kuwa kuendeleza ujasiriamali endelevu na usimamizi bora wa biashara ndogo na za kati ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya uvuvi na uchumi wa taifa. Aidha, alitoa mapendekezo kwa serikali na wadau wa sekta ya uvuvi ili kuimarisha biashara ndogo na za kati kwa njia endelevu na yenye tija, hatua itakayosaidia kukuza uchumi na maendeleo ya jamii. mwenyekiti wa jopo la watahini, Prof. Ernest Kihanga, baada ya mjadala wa kina, alitangaza kuwa Bi. Mwanahamisi Salehe amefanikiwa kwa kiwango cha kuridhisha kutetea tasnifu yake, akibainisha kuwa matokeo ya utafiti wake yana mchango mkubwa katika kuendeleza sekta ya uvuvi nchini. Hatua hii inaendelea kuthibitisha nafasi ya Chuo Kikuu Mzumbe kama nguzo muhimu ya tafiti zenye tija kwa maendeleo ya taifa.