News-Details

News >Details

KIKAO CHA WARATIBU WA HEET CHASISITIZA KASI NA UFANISI WA UTEKELEZAJI

KIKAO CHA WARATIBU WA HEET CHASISITIZA KASI NA UFANISI WA UTEKELEZAJI

Ili kuhakikisha Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeandaa kikao maalumu cha waratibu wa mradi huo kwa taasisi zote zinazofaidika, kilichofanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia Septemba 15 hadi 19, 2025. Kikao hicho kimewaleta pamoja waratibu kutoka vyuo vikuu na taasisi mbalimbali kwa lengo la kujadili mwenendo wa utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati unaolenga kuboresha elimu ya juu nchini. Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Nelson Boniface, alieleza kuwa kikao hicho ni fursa ya kipekee ya kujenga mshikamano na mshirikiano miongoni mwa taasisi nufaika, pamoja na kubadilishana uzoefu, changamoto na mipango ya utekelezaji. Kwa upande wake, Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa HEET, Dkt. Kennedy Hosea, alieleza kuwa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 74.3 na kupongeza jitihada za waratibu wote na Kamati ya Utekelezaji wa Mradi (PIC) kwa kazi kubwa iliyofanyika hadi sasa. Naye Naibu Mratibu wa Kitaifa, Dkt. Evaristo Mtitu, alieleza nafasi na mchango wa kila taasisi katika utekelezaji, jambo lililosaidia kuimarisha mshikamano wa pamoja katika kufanikisha malengo ya HEET. Katika kikao hicho, waratibu walipokea taarifa za maendeleo ya miradi ikiwemo mpango endelevu wa taasisi baada ya mradi kukamilika, taarifa za ukaguzi wa ndani na mrejesho wa CAG, maendeleo ya usomeshaji wa watumishi, maandalizi ya awamu ya ufungaji wa mradi, pamoja na hatua za kusaidia watumishi kukamilisha masomo yao. Miongoni mwa waliowasilisha mada ni Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Lihoya Chamwali, ambaye aliwasilisha taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu kwa mwaka Septemba 2024 hadi Septemba 2025, sambamba na ripoti ya masuala ya kijamii na kimazingira, hali ya upakiaji wa kazi kupitia mfumo wa STEP, na utekelezaji wa hoja za ukaguzi. Kwa ujumla, kikao hiki kimetajwa kuwa chachu ya kuimarisha mikakati na kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi, huku washiriki wakihimizwa kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha Mradi wa HEET unakamilika kwa wakati na kuleta mageuzi tarajiwa katika elimu ya juu nchini Tanzania.

None
None
None
None
None