Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya kimekuwa mwenyeji wa kongamano kubwa kuhusu uchumi jumuishi lenye mada kuu: "Mwenendo wa Uchumi Tanzania Kuelekea Dira 2050”. Kongamano hilo lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia (PPP Centre), lilifanyika tarehe 18 Septemba 2025 kwenye ukumbi wa Nkuramah - Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya na kuhudhuriwa na wageni wapatao 500 wakiwemo wakuu wa mikoa, wakurugenzi wa wilaya, makatibu tawala, viongozi wa dini, wakuu wa taasisi binafsi na wawakilishi wa vyuo vikuu. Kongamano hilo lililenga kuelimisha umma kuhusu Dira ya Taifa ya 2050, kupitia upya mpango wa maendeleo unaoishia na kuweka mikakati ya utekelezaji wa dira mpya. Pia, kongamano hilo lililenga kuchambua nafasi ya ubia kati ya sekta binafsi na serikali katika kufanikisha Dira 2025 na kutekeleza jitihada za maendeleo kuelekea mwaka 2050 kwa kuangazia changamoto, fursa na mwelekeo wa kiuchumi katika Taifa. Akitoa salamu za ukaribisho kwa niaba ya Chuo Kikuu Mzumbe, Naibu Rasi wa Ndaki ya Mbeya, Prof. Charles Tundui, aliwashukuru waandaaji kwa kuchagua Ndaki ya Mbeya kuwa mwenyeji wa kongamano hilo kubwa. “Hii ni heshima kubwa kwa Chuo chetu na tunajivunia kupewa nafasi hii adhimu ya kushirikiana na taasisi kongwe kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Kituo cha Ubia,” alisema Prof. Tundui. Kongamano hilo liliongozwa na Mwenyekiti wake, Prof. Alexander Makulilo, ambaye alifungua mjadala wa mada kuu na kutoa nafasi kwa wachambuzi na wajadili mada. Washiriki walipata nafasi ya kuuliza maswali na kutoa maoni, jambo lililoongeza mvuto na kina cha majadiliano. Naye, Dkt. Jasinta Kahyoza, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya na mtoa mada alieleza kuwa, kuwepo kwa ajira, mazingira bora ya biashara na uwekezaji ndio kiu kubwa ya sekta binafsi. Pia, alibainisha eneo la miundombinu ni muhimu sana na ni jukumu la serikali. Sasa Kituo cha Ubia(PPPC) kinatoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki kukuza uchumi wa nchi. Kiini kikubwa cha ubia ni kihakikisha kuwa sekta binafsi, serikali na wananchi wananufaika. Hivyo, ni muhimu kwa wananchi wote kushiriki katika utekelezaji wa Dira 2050. Akihitimisha rasmi kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Ubia, Bw. David Kafulila, aliushukuru na kupongeza uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya kwa maandalizi mazuri na ukarimu waliouonesha. “Nichukue nafasi hii kipekee kabisa kuupongeza uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya kwa kuthibitisha ukomavu wenu licha ya taarifa ya muda mfupi. Nikiwa mzaliwa wa Mzumbe kitaaluma, najivunia kuwa zao la Chuo hiki,” alisema Bw. Kafulila kwa msisitizo. Kongamano hili limeacha alama ya pekee katika historia ya Chuo Kikuu Ndaki ya Mbeya na kuonesha mchango mkubwa wa vyuo vikuu nchini katika kuunga mkono jitihada za Serikali kuelekea kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.